
Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mhe Damasi Ndumbaro akizungumza wakati wa Mafunzo ya sita na mawakili zaidi ya 600 kutoka Wizara, taasisi na mamlaka mbalimbali ya umma
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa Sheria za Nchi haziendi likizo kipindi cha kampeni za uchaguzi bali zinakuwepo na zinapaswa kufuatwa kama inavyotakiwa.
Ndumbaro ameyasema hayo leo Juni 03, 2025 wakati akifungua Mafunzo ya Sita ya mawakili wa serikali zaidi ya 600 kutoka Wizara,Taasisi na Mamlaka mbalimbali za umma .
“Mwaka huu ni Mwaka wa uchaguzi, Kuna mengi tutayasikia, Lakini katika kipindi hiki cha Kampeni Mimi hua najiuliza sana, hivi Sheria zinakwenda likizo? Kwasababu tunataka kuaminishwa uvunjifu wa Sheria utakaotokea kipindi cha kampeni sio uvunjifu wa Sheria kwasababu tu unafanywa na wanasiasa, kwa uelewa wangu wa sheria nasema kipindi cha kampeni Sheria haziendi likizo, Sheria zipo zinafanya kazi, wanasheria wapo wanafanya kazi, Mahakama zipo zinafanya kazi”, amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Aidha Mhe. Ndumbaro amewataka mawakili hao kuwaelimisha wanasiasa juu ya kuzingatia Sheria katika kipindi cha Kampeni Kama ambavyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 13 (1) inavyozungumzia usawa mbele ya sheria.
Ameongeza kuwa mwanasiasa ama mtu yeyote atakaye kiuka sheria za nchi katika kipindi cha kampeni atahesabika mhalifu kama wahalifu mwengine, kwani uchaguzi ni zoezi la kikatiba.
Social Plugin