Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHENGERWA ATANGAZA KUVUNJA RASMI MABARAZA YA MADIWANI NCHI NZIMA! ....'WATABAKI NA VISHIKWAMBI'




Na Woinde Shizza, Arusha

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, ametangaza rasmi kuvunjwa kwa mabaraza yote ya madiwani nchini huku akiwasihi viongozi hao kuendelea kulinda amani na kuyatangaza mafanikio ya serikali ya Awamu ya Sita.

Waziri Mchengerwa alitoa tamko hilo leo Juni 20, 2025 kwa njia ya simu kupitia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa Jiji la Arusha, akisema kuwa tamko hilo ni kwa ajili ya mabaraza yote nchini.

Katika hotuba hiyo, Mchengerwa aliwapongeza madiwani kwa utendaji wao mzuri na kueleza kuwa kazi yao imeandikwa kwenye kitabu cha dhahabu kwa namna walivyotekeleza majukumu yao kwa weledi.

“Nawashukuru kwa kazi yenu nzuri,mmefanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya sita mafanikio mengi yaliyopatikana yametokana na ushirikiano wenu,” alisema Mchengerwa.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI kuhakikisha kuwa madiwani waliokuwa madarakani wanabaki na vitendea kazi walivyokabidhiwa na serikali, ikiwemo vishkwambi, kwa kuwa vifaa hivyo havitakiwi kurudishwa halmashauri.

“Vifaa walivyotumia madiwani kama vishkwambi wabaki navyo kwa sababu vina taarifa binafsi na si mali ya halmashauri,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, aliwataka madiwani kuhakikisha wanasimamia amani katika maeneo yao na kuepuka kuhusika na vurugu, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
Aidha, Makonda aliagiza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo pamoja na wakurugenzi wengine kuhakikisha madiwani wanalipwa stahiki zao kwa wakati ili waweze kuendelea na shughuli zao za kisiasa na maisha ya kawaida.


Makonda pia aliwaomba madiwani hao kuendelea kuisemea serikali kwa mazuri yote yaliyotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alimwelezea kama kiongozi aliyefanikisha mageuzi ya kiuchumi nchini.

“Ni wajibu wenu kusimulia mema yote yaliyofanywa na Rais Samia. Serikali yake imeleta mafanikio makubwa katika maendeleo,” alisema.

Viongozi wa serikali za mitaa na vitongoji pia waliagizwa kuhakikisha wanalipwa posho zao kupitia akaunti zao binafsi na si kwa kupitia watendaji wa kata, sambamba na kushirikishwa ipasavyo katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com