Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WENYE ULEMAVU WATAKA KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Wakati Serikali ikijiandaa kuanza utekelezaji wa Sheria mpya ya Bima ya Afya kwa Wote, wito umetolewa kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika upatikanaji wa huduma bora za afya.

Wadau mbalimbali wamehimiza Serikali kutazama kundi hilo kwa jicho la kipekee ili kuhakikisha kuwa mahitaji yao ya kipekee yanazingatiwa kikamilifu.

Akizungumza katika mkutano wa kitaifa wa mashauriano kuhusu Mgao wa 30% wa Samia kupitia mfumo wa NeST kwa watu wenye mahitaji maalum, uliofanyika jijini Dodoma, Muasisi wa Ikupa Trust Fund, Stella Ikupa, amesisitiza kuwa licha ya juhudi za Serikali kuboresha huduma za afya, watu wenye ulemavu bado wanakumbwa na changamoto lukuki.

"Ukosefu wa vifaa saidizi, miundombinu isiyofikika, pamoja na upungufu wa watumishi wa afya waliobobea kuwahudumia watu wenye ulemavu, ni baadhi ya vikwazo vinavyowafanya washindwe kufurahia haki yao ya msingi ya kupata huduma za afya," amesema Bi. Ikupa.

Amesema kuwa mpango wa bima ya afya kwa wote hauwezi kuwa jumuishi bila kuzingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu.

Amegusia pia umuhimu wa ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika michakato ya kisiasa hasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao huku akisisitiza uwepo wa wakalimani wa lugha ya alama kwenye kampeni, mikutano ya hadhara, na matangazo ya moja kwa moja ya kisiasa ili kuhakikisha usawa wa upatikanaji wa taarifa.

Ikupa pia amepongeza Shirika lake na wadau wakiwemo PPRA kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuwapatia vifaa saidizi, elimu ya haki zao, na mafunzo ya kujitegemea.

Pia ametoa shukrani kwa Serikali kwa kutenga mgao maalum wa asilimia 30 kwa makundi maalum katika mchakato wa manunuzi ya umma.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete, amesema kuwa Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Ameeleza kuwa tayari Serikali inatenga fedha kusaidia vikundi vya watu wenye ulemavu, inajenga shule jumuishi na kuboresha sera ya elimu ili iendane na mahitaji yao.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutoa mafuta maalum kwa watu wenye ualbino ili kuwalinda dhidi ya saratani ya ngozi, na kuahidi usimamizi madhubuti wa sera na mikakati inayolenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kijamii na kiuchumi.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa PPRA, Winfrida Samba, alibainisha kuwa mfumo wa NeST umewezesha watu 1,335 wenye ulemavu kusajiliwa kama wazabuni kwenye kanzidata ya serikali.

"Hili limeongeza uwazi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa manunuzi ya umma" ameeleza.

Wadau wametoa rai kwa mashirika ya kiraia na Serikali kushirikiana kwa karibu kuhakikisha kuwa sera mpya ya Bima ya Afya kwa Wote inatekelezwa kwa namna itakayojumuisha kila Mtanzania bila ubaguzi.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com