Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Serikali imeendesha kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Usawa wa Kijinsia, kilicholenga kutathmini mafanikio, changamoto na hatua zilizochukuliwa katika kuimarisha usawa wa kijinsia nchini.
Kikao hicho, kilichofanyika katika ukumbi wa Domiya Estate jijini Dodoma, kimewaleta pamoja washiriki zaidi ya 65 kutoka serikalini, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Mageuzi ya Usawa wa Kijinsia (2021–2027) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).
Akizungumza kwenye kikao hicho leo Mei 29,2025 Jijini hapa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju, amesema kikao hicho kimechochea mijadala muhimu kuhusu sababu za kiwango cha chini cha utoaji taarifa za ukatili wa kijinsia, pamoja na mikakati ya kuboresha huduma za madawati ya kijinsia mashuleni na kwenye jamii.
“Tunaendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu namna wanawake wanavyoshiriki katika uchumi na jamii kwa ujumla,tunataka kuona matakwa ya kikatiba kuhusu usawa wa kijinsia yanatekelezwa kwa vitendo,” amesema Mpanju.
Ameongeza kuwa licha ya uwepo wa sheria zinazolinda haki za wanawake, utekelezaji wake unakumbwa na changamoto za kimfumo, hivyo Serikali inashirikiana na wadau kusukuma mbele ajenda ya usawa.
“Tuna Madawati ya Polisi ya Jinsia na Watoto ambayo ni maeneo salama kwa waathirika wa ukatili,tunaendelea kuhakikisha huduma hizi zinakuwa rafiki na bora kwa jamii,” amesema
Kwa upande wake, Karina Dzialowska ambaye ni Mkuu wa Idara ya Uchumi na Utawala Bora wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, amesema miaka miwili ya utekelezaji wa mpango huu imeleta mafanikio yanayoonekana, huku akieleza dhamira ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Amesema Mpango huo wa miaka saba unalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha, kupambana na ukeketaji na ndoa za utotoni, na kuwawezesha wanawake kupitia taasisi kama PWC, ELCT, na mfuko wa TASAF.
"Ili kufanikiwa hili, Umoja wa Ulaya umetenga Euro milioni 90, ambapo Euro milioni 28 zinaenda moja kwa moja kwenye bajeti ya Serikali ya Tanzania, na Euro milioni 7 zimeelekezwa Zanzibar kwa ushirikiano na UN Women, " amesema.
Naye Mtakwimu wa Wizara hiyo na Mratibu wa mradi Alex Shayo, amesema ripoti zinaonyesha kupungua kwa kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto kutoka asilimia 40 mwaka 2017 hadi asilimia 27 hivi sasa.
“Takwimu hizi zinaonyesha kuwa sasa jamii imeanza kuelewa haki na wajibu wake, na watu hawana hofu tena ya kuripoti ukatili,” amesema Shayo.
Hata hivyo amesema Serikali imeanzisha nyumba salama na madawati ya kijinsia kutoa msaada wa kisheria na kisaikolojia wakiwemo wanaume waathirika huku changamoto kubwa zinatajwa kuwa mila kandamizi, ukosefu wa maeneo salama kwa waathirika na mfumo wa utekelezaji wa sheria ambao bado haujawafikia kikamilifu wahanga wote.
Lucy Uisso, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, amesema kuwa ongezeko la kesi za ukatili zinazofikishwa mahakamani linaonesha kuwa jamii sasa ina imani na mfumo wa haki.
“Wengi wanaohukumiwa kwa makosa ya ubakaji ni wanaume, na hii inaonesha kuwa haki inatendeka,” amesema Uisso na kuongeza;
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wafungwa waliopo magerezani kwa makosa ya ubakaji inaongezeka, jambo linalodhihirisha utendaji wa vyombo vya haki, "amesisitiza .
Amesisitiza kuwa mafanikio ya kupambana na ukatili wa kijinsia hayawezi kuletwa na Serikali pekee Bali Jamii nzima inahimizwa kushiriki katika kutoa taarifa, kuelimishana, na kuwawezesha wanawake na watoto kupata haki zao bila woga.
Social Plugin