
Meneja wa MBIFACU (Mbinga Farmers Co-operative Union Ltd)Faraja Komba akimkaribisha mgeni rasmi mrajisi Msaidizi Mkoa wa Ruvuma Peja Muhoja katika Mafunzo ya wenyekiti na watendaji wa vyama vya ushirika vilivyopo chini ya mwamvuli wa MBIFACU

Wenyekiti na watendaji wakimsikiliza mgeni rasmi Mrajis Msaidizi Mkoa Peja Muhoja pichani hayupo

Na Regina Ndumbaro Mbinga, Ruvuma
Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma, Peja Muhoja, ametoa wito mzito kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika chini ya mwamvuli wa MBIFACU kuhakikisha wanasimamia wajibu wao ipasavyo, wakiepuka uzembe, migogoro, na vitendo vya kuhujumu uchumi wa wakulima.
Akizungumza katika mafunzo ya Watendaji wa vyama vya ushirika yaliyofanyika katika ukumbi wa Mbicu Hotel Wilayani Mbinga, Muhoja amesisitiza umuhimu wa ubora wa kahawa, uwajibikaji wa viongozi, na usimamizi madhubuti wa Uingiaji wa mikataba ya uuzaji wa Kahawa.
Muhoja ameeleza kuwa baadhi ya vyama vimekuwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kutowalipa wakulima kwa Wakati na viongozi kutotekeleza majukumu yao ipasavyo.
Amesema Soko la awali linalofanyika kupitia Mikataba limegeuzwa kuwa kichaka cha kuweka bei zisizo rasmi kwa manufaa binafsi.
Ameonya kuwa msimu ujao mikataba yote ya Soko la awali isiyopitishwa na chama cha MBIFACU haitatambuliwa katika Ofisi yake.
Pia kupitia hotuba hiyo, Muhoja amekemea vikali matumizi ya kile alichokiita “magoma” – watu wanaotumiwa kuhujumu mfumo wa ushirika kwa manufaa ya wachache.
Amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi wanaoendekeza tabia hizo, na kwamba kila chama kinapaswa kuwa na nidhamu, kuelewa wajibu wake, na kuhakikisha fedha za wanachama zinawekwa kwenye benki ya ushirika kama ili kuhakikisha usalama wa fedha hizo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwasilisha taarifa za utendaji kwa wakati, kukamilisha miongozo, kutumia mfumo wa MUVU na kuhakikisha kila Chama kinaandaa mpango mkakati kwaajili ya matumizi kama Dira ya Chama.
Mwisho amewaasa viongozi kujifunza kutoka kwa viongozi wakuu wa nchi katika kuonyesha uwajibikaji, nidhamu na uadilifu katika utendaji kazi wa kila siku.
Social Plugin