Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE ULENGE AIOMBA SERIKALI KUTOA FEDHA KWA WAKATI KUKUZA UZALISHAJI MKONGE




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalum, Mwanaisha Ulenge (CCM), ameiomba Serikali kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi wa kituo atamizi cha uzalishaji wa bidhaa za mkonge zinawafikia walengwa kwa wakati, hususan vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Akizungumza bungeni leo Mei 22, 2025 wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Ulenge amesema Serikali tayari imetenga Shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kituo hicho, lakini hatua madhubuti zinahitajika kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wa haraka na wenye tija.

“Tunawashukuru sana, tunaishukuru Bodi ya Mkonge ya Tanga. Naomba sana Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ihakikishe milioni 600 zinafika kwa wakati ili tuweze kukuza uchumi wetu,” amesema Ulenge.

Amesisitiza kuwa ni muhimu bidhaa zitokanazo na mkonge zizalishwe kwa wingi ili zitumike ndani ya nchi na pia katika masoko ya kimataifa, jambo litakalosaidia kuongeza thamani ya zao hilo na kuinua maisha ya vikundi vinavyoshiriki katika mradi huo.

Aidha, ametoa rai kwa Serikali kuendeleza mikakati ya kuwajengea uwezo vijana na wanawake wanaojihusisha na kilimo cha mkonge, ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu ya biashara, vifaa vya kisasa na fursa za mitaji ili waweze kuongeza uzalishaji na ushindani katika soko la dunia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com