Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAGEUZI MAPYA KATIKA SEKTA YA MILIKI YALENGA KUIMARISHA MAKAZI NA BIASHARA



Na Woinde Shizza, Arusha

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iko mbioni kuandaa sera mpya pamoja na kupitia sheria mbalimbali zitakazotambua kada ya Miliki, Wathamini na Madalali nchini.

Akizungumza jijini Arusha katika mkutano wa tano wa mwaka wa wadau wa Miliki Kuu, Waziri wa wizara hiyo, Deogratius Ndejembi, amesema kuwa serikali imelenga kuimarisha sekta ya makazi na kupanua wigo wa biashara.

Amesema mchango wa wataalamu wa miliki ni mkubwa katika kukuza na kuimarisha miundombinu ya nchi, jambo linalokwenda sambamba na dhamira ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mageuzi haya yanaendana na maboresho ya miundombinu kama Reli ya Kisasa, barabara, usafiri wa anga na maji,” amesema Ndejembi, huku akiahidi ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wataalamu wa sekta hiyo.

Rais wa Chama cha Wataalamu wa Miliki Kuu nchini, Andrew Kato, amesema kutokuwepo kwa sera maalumu ya makazi kumechangia changamoto nyingi katika sekta hiyo na kuathiri utekelezaji wa miradi.
Amesema sera na sheria mahususi zitasaidia kuweka mipaka ya majukumu, kurahisisha huduma kwa wananchi, na kuhakikisha kuwa miradi inakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa.

Makamu wa Rais wa Miliki Afrika Mashariki, Prof. Nicky Nzioki, ameshauri serikali kuiga mifumo ya nchi kama Kenya na Rwanda katika usimamizi wa sekta ya makazi, akibainisha kuwa sera hiyo ikiwekwa itasaidia pia kuongeza ajira kwa vijana.

Mkutano huo umehudhuriwa na zaidi ya washiriki 180 kutoka kada mbalimbali ikiwemo Maafisa Ardhi, Wathamini, Wasimamizi wa Majengo, Wawekezaji na Wataalamu wa sekta ya miliki kutoka nchi za Afrika Mashariki

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com