Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Hassan Linyama akitoa Elimu ya Msaada wa kisheria wa Mama Samia (Samia Legal Aid)
Wananchi wa Kata ya Mtyangimbole wakipata Elimu ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro Madaba-Songea
Katika juhudi za kuendeleza utawala wa sheria na kulinda haki za binadamu, kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (Samia Legal Aid) umezinduliwa rasmi katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.
Kampeni hii ya kitaifa inalenga kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi, ikiwemo masuala ya ukatili wa kijinsia, mirathi, uraia, uchaguzi na utatuzi wa migogoro.
Wananchi wa kata ya Mtyangimbole wamekuwa wa kwanza kunufaika na elimu hiyo, ambapo mafunzo hayo yamefanyika katika shule ya sekondari ya Luhimba na shule ya msingi ya Mtyangimbole.
Elimu hiyo imetolewa na jopo la wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria lkiongozwa na Wakili wa Serikali, Bw. Hasan Linyama, ambaye ameongoza mafunzo hayo kwa weledi mkubwa.
Kampeni hii imeandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na Mbunge wa Jimbo la Madaba, Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wake wanapata uelewa wa haki zao kisheria na namna ya kushughulikia changamoto za kijamii na kifamilia.
Kwa muda wa siku kumi, kampeni hii itaendelea katika kata tatu za Halmashauri ya Madaba ambazo ni Mtyangimbole, Luhimba na Likarangiro.
Mafunzo haya yameelekeza zaidi katika kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa kingono, ukatili wa kiuchumi na hata vitendo vinavyopelekea vifo kutokana na ukosefu wa maarifa ya kisheria.
Aidha, wananchi wamepata mafunzo ya msingi kuhusu utawala bora na ushiriki wa wananchi katika chaguzi za kidemokrasia.
Wananchi ambao wamehudhuria elimu hiyo, akiwemo Hamisi Chilemba Msusa na Oresta Mhagama, wameeleza furaha yao kwa kupata maarifa haya muhimu.
Wamesema elimu hiyo imewasaidia kuelewa haki zao, namna ya kulea watoto katika misingi ya haki, na pia jinsi ya kushughulikia migogoro ya kifamilia kwa njia ya amani.
Wameeleza kuwa hapo awali walikuwa hawajui pa kuanzia katika kutafuta suluhisho la changamoto zao, lakini sasa wamefunguliwa macho kisheria.
Wananchi wa Madaba wamempongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mpango huu wa msaada wa kisheria ambao unawagusa watu wa ngazi zote, mijini na vijijini.
Pia wametoa pongezi kwa Mheshimiwa Mbunge Joseph Kizito Mhagama kwa kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wa jimbo lake.
Wameomba mafunzo haya yawe endelevu ili kuendelea kuwaelimisha watu wengi zaidi kuhusu haki, wajibu na sheria za nchi.
Social Plugin