Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

FAHARI MPYA YA DODOMA:JENGO LA KISASA LA CCM KUINUA MANDHARI YA JIJI




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Dodoma yazidi kung’ara kama kitovu cha kisiasa na maendeleo nchini, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo jipya la kisasa la Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mradi huo mkubwa utagharimu takribani shilingi bilioni 34.13 hadi kukamilika, na linatarajiwa kuwa jengo la ghorofa tano, lenye kuchangia katika kuboresha mandhari ya mji wa serikali na kuongeza hadhi ya chama hicho kikongwe.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika leo Mei 28,2025 jijini Dodoma, Rais Samia amesema ujenzi huo ni hatua muhimu ya kutimiza ndoto ya muda mrefu ya CCM, ndoto iliyobebwa tangu enzi za waasisi wa chama.


“Tulilolikusudia kwa miaka mingi leo limetimia. CCM ni chama cha maendeleo ya watu, na wananchi wameonyesha mshikamano wao kwa kujitolea maeneo kwa ajili ya mradi huu,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa hatua ya kuhusisha kampuni za ndani ni kielelezo cha kuamini uwezo wa Watanzania, akisisitiza kuwa jengo hilo linapaswa kuakisi ubora, uzalendo, na maadili ya CCM.

“Tumekubaliana, sasa tunatekeleza,hii ndiyo maana ya chama chenye uamuzi na mshikamano,” amesisitiza.

Rais Samia amesisitiza kuwa jengo hilo halipaswi kuchukuliwa kama tu alama ya utawala, bali mahali pa kuibua vipaji, kujifunza uongozi, na kulea kizazi kipya cha viongozi waadilifu.

Aidha, ametangaza kufunguliwa rasmi kwa dirisha la wanachama kuchangia kwa hiari ujenzi huo, ili kuongeza ushiriki na kuwapa wanachama nafasi ya kuwa sehemu ya miradi ya chama chao.

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameeleza kuwa jengo hilo ni utekelezaji wa ndoto ya mwaka 1977, na linaashiria mwanzo mpya kwa chama katika karne hii ya mageuzi.

“Hili si tu jengo la kifahari, ni alama ya ukuaji wa CCM na nafasi yake kama kinara wa mabadiliko ya kijamii na kisiasa,” amesema.

Amebainisha kuwa fedha za awali kiasi cha shilingi bilioni 8 tayari zipo, na ujenzi unatarajiwa kukamilika kabla ya jubilei ya chama mwaka 2027.

Naye Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, ametaja mradi huo kama “mchoro hai wa maono ya uongozi wa Rais Samia,” akisema ni moja ya alama kubwa anazoziacha ndani ya chama.

“Ujenzi huu si tu kuhusu jengo, bali ni ujenzi wa imani, umoja na maono mapya ya CCM.”amesema










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com