Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BODABODA KUPATA MATAIRI MAPYA KWA MKOPO HATUA ITAKAYO PUNGUZA AJALI NA KUKUZA UCHUMI




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Waendesha bodaboda na bajaji nchini wamepata afueni kubwa baada ya kuzinduliwa kwa kampeni ya kitaifa ya kuwawezesha kupata matairi mapya kwa mkopo wa kulipa kidogo kidogo kuanzia shilingi 10,000.

Kampeni hiyo, ijulikanayo kama "Gurudumu la Mama", inalenga kuinua usalama barabarani na kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana wanaojishughulisha na sekta ya usafirishaji.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amezindua rasmi mpango huo jijini Dodoma leo Mei 28,2025 na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kutatua changamoto za vijana nchini.

“Mara nyingi ajali husababishwa na matairi chakavu,kupitia kampeni hii, tunataka madereva wetu wafanye kazi kwa usalama na kujiamini,” amesema Mhe. Senyamule.

Kampeni hii inalenga kupunguza ajali zinazotokana na ubovu wa matairi, hususan kwa bodaboda ambao wamekuwa wahanga wakubwa wa ajali nchini.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka vyombo vya usalama barabarani, matairi mabovu ni miongoni mwa visababishi vikuu vya ajali za pikipiki mijini na vijijini.

RC Senyamule ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa waendesha bodaboda kuepuka matumizi ya pombe wakati wa kazi, akieleza kuwa matumizi ya kilevi mchana ni miongoni mwa sababu kuu za ajali.

“Kama huwezi kuacha pombe, basi usitumie wakati wa kazi. Uhai wa abiria na wenu uko mikononi mwenu,” ameonya Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma

Ameongeza kuwa madereva wana nafasi kubwa ya kiuchumi kupitia bodaboda, hasa katika jiji la Dodoma ambalo hufanya shughuli nyingi za mikutano ya kitaifa.

Senyamule amewataka vijana kujiunga na vyama vyao vya usafirishaji ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali na wadau wa maendeleo.

Pia amewahimiza kuweka akiba na kuwa waaminifu kazini, akisema nidhamu ya kazi ndiyo msingi wa mafanikio.

“Usalama wenu ni msingi wa maisha yenu. Matairi mazuri si anasa, ni uhai. Jilindeni, jilinde abiria, jitenge na ajali,” amehitimisha.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri, amesema yeye binafsi ni mhanga wa ajali iliyosababishwa na tairi chakavu, na kuwataka madereva kuzingatia ukaguzi wa usalama wa vyombo vyao kabla ya kazi kila siku.

Mratibu wa kampeni hiyo, Thuweni Makamba, amesema Mpango huo unaendeshwa kwa ushirikiano na kampuni ya utengenezaji wa matairi ya Road Master, ambapo matairi yatatolewa kwa mkopo kwa udhamini wa vyama vya waendesha bodaboda na bajaji.

Amesema wameamua kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza kauli mbiu ya “Gurudumu la Mama – Matairi Mapya, Usalama Mpya”.

“Rais ni mdau wa sekta binafsi, na sisi tumeona tutoe mchango wetu kwa vijana kupitia njia hii ya moja kwa moja ya kiuchumi,” ameeleza Makamba.

Kwa upande wake Mbunge wa Dodoma Mjini, Mh.Anthony Mavunde, amepongeza mpango huo na kutangaza kuanzisha SACCOS ya bodaboda ifikapo tarehe 5 Juni mwaka huu ili kuwawezesha kupata mikopo yenye masharti nafuu.

“Tutaanza na zaidi ya waendesha bodaboda elfu moja na kuweka mfuko wa fedha za maendeleo kwao,lengo ni kuondoa kikwazo cha mitaji midogo kwa vijana hawa,” amesema Mavunde.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com