
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rechal Kassanda akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyasa Wilayani Masasi wakati Mwenge wa Uhuru ulipowasili Wilayani humo
Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara
Wakazi wa Kata ya Nyasa, Halmashauri ya Mji wa Masasi, wamehimizwa kuitunza barabara mpya iliyojengwa katika eneo lao, ikiwa ni sehemu ya jitihada za maendeleo zinazoletwa na serikali.
Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndugu Ismail Ally Ussi, mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika barabara hiyo mpya wakati wa mbio hizo kuwasili katika halmashauri hiyo.
Mwenge wa Uhuru kwa sasa upo katika Wilaya ya Masasi na umeanza mbio zake ndani ya Halmashauri ya Mji wa Masasi.
Katika wilaya hiyo, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kwa umbali wa kilomita 181.4 na utapitia halmashauri mbili tofauti.
Mbio hizo zimepangwa kugusa maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tarafa saba, Kata kumi na sita, Vijiji thelathini na sita pamoja na mitaa kumi na sita.
Akiwa katika Halmashauri ya Mji wa Masasi, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupita kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni nne.
Miradi hiyo inahusisha sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, afya, elimu na maji, ikilenga kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo hayo.
Wakazi wa Kata ya Nyasa wameeleza furaha na shukrani zao kwa Serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo ambayo wamesema itarahisisha shughuli za usafirishaji na kuinua uchumi wao kwa ujumla.
Wamesema barabara hiyo itawasaidia wakulima na wafanyabiashara kusafirisha bidhaa kwa urahisi na kuongeza tija katika shughuli zao za kila siku.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ndugu Ismail Ally Ussi, pia ametumia fursa hiyo kuwasihi wakazi wa Wilaya ya Masasi kushiriki kwa amani katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano katika kipindi chote cha uchaguzi kwa maendeleo endelevu ya taifa.


Social Plugin