
Salfa zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wakulima wa korosho Nachingwea Mkoani Lindi

Baadhi ya wakulima wa Nachingwea Mkoani Lindi wakibeba salfa walizogawiwa na Mwenyekiti wa Runal Amcos ,Odas Mpunga kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wakulima wa zao la korosho



Na Regina Ndumbaro Nachingwea-Lindi
Wakazi wa Kijiji cha Palamtua na Farm Seventeen, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, wameeleza furaha yao baada ya kupokea tani 3,000 za salfa zilizotolewa bure kwa wakulima wa korosho.
Wamesema msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo muhimu kiuchumi katika eneo lao.
Mwenyekiti wa Runali Amcos, Ndg. Odas Mpunga, amesema wakulima wa maeneo hayo wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia pembejeo hizo bila malipo.
Amesema hatua hiyo ni ishara ya wazi kuwa serikali inajali wakulima na inatambua mchango wao katika uchumi wa taifa.
Mpunga ameeleza kuwa ugawaji wa salfa hizo kwa wakulima utasaidia kuimarisha kilimo cha korosho, kwa kuwa pembejeo hizo ni muhimu katika kudhibiti magonjwa na wadudu wanaoshambulia mikorosho.
Ameongeza kuwa wakulima sasa wana matumaini makubwa ya kupata mazao bora na yenye tija msimu huu.
Kwa upande wake, mkulima Noel Mmole kutoka Kijiji cha Farm Seventeen naye ametoa shukrani zake kwa Rais Samia kwa kutoa pembejeo hizo bure.
Amesema kuwa hatua hiyo imerahisisha kazi yao kama wakulima na itaongeza kipato cha kaya nyingi kutokana na ongezeko la uzalishaji wa korosho.
Social Plugin