Waziri wa Katiba na Sheria pia Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mhe. Damas Ndumbaro akizungumza na wananchi wa Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea wakati wa Mwenge wa Uhuru ukiweka jiwe la msingi wa mradi wa maegesho ya Magari

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amewakumbusha wananchi kuhusu umuhimu wa kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi sambamba na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maegesho ya magari ya malori katika Kata ya Lilambo, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa uchaguzi mkuu utafanyika kama kawaida na hakutakuwa na kauli ya “no reform no election”.
Aidha, amewasisitiza wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi kwa kuzingatia elimu ya kujikinga.
Kwa upande wake, kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Ismail Ussi, ameeleza kuridhishwa na maendeleo yanayoendelea kutekelezwa kwa kasi katika Manispaa ya Songea.
Amepongeza juhudi za viongozi wa Manispaa hiyo kwa kufuata maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha miradi yenye tija inatekelezwa na kudumu.
Amesema serikali inahimiza ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuinua hali ya maisha ya wananchi.
Ismail Ussi amebainisha kuwa mradi wa ujenzi wa maegesho ya magari ya mizigo ni wa kimkakati na utaleta tija kwa Manispaa ya Songea.
Amesema uwepo wa maegesho hayo yatasaidia kuimarisha huduma mbalimbali ikiwemo mapumziko, chakula, malazi, ajira kwa wananchi, na kuongeza mapato kwa Manispaa.
Aidha, amehimiza wananchi kushirikiana na watendaji wa serikali ili kulinda na kutunza miundombinu hiyo muhimu.
Kiongozi huyo wa mbio za mwenge amesema ameshuhudia mafanikio mengi katika eneo hilo ambayo yanadhihirisha kasi ya maendeleo chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais.
Ameongeza kuwa matarajio ya Mbunge wa Jimbo la Songea kuona mji huo unakuwa jiji ni halali na yanaweza kutimia kwa kuzingatia utekelezaji wa miradi mikubwa kama hiyo.
Amewasihi viongozi wa Manispaa na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa mradi huo wa maegesho unakamilika kwa wakati na kwa viwango vya ubora vilivyowekwa.
Amesema mradi huo ni kielelezo cha maendeleo na kwamba unapaswa kutunzwa kama rasilimali muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Social Plugin