
Baadhi ya Wajumbe wa bodi waliopata elimu hiyo ya mkakati ya kudhibiti udanganyifu wa mizani wa AMCOS Mbinga na Nyasa
Meneja wa wakala wa vipimo Mkoa wa Ruvuma Edward Mkanjabi akiwa anatoa elimu ya mikakati ya kukomesha udanganyifu wa mizani AMCOS Mbinga na Nyasa
Na Regina Ndumbaro Mbinga -Ruvuma
Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoa wa Ruvuma, Edward Mkanjabi, amezungumzia changamoto mbalimbali zilizobainika katika ukaguzi wa mizani ya vyama vya ushirika (AMCOS) wilayani Mbinga, katika mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mbicu Hotel.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Meneja ameeleza kuwa mizani mingi imekutwa ikiwa imekatwa lakiri ya Serikali( seal) ambayo hufungwa kwa lengo la kuzuia uchezeaji wa mizani na kuhakikisha usahihi wa Vipimo.
Baadhi ya changamoto kuu zilizobainika ni pamoja na vyama vya ushirika kutumia mizani ambayo haijahakikiwa na kutumia mizani duni ambazo haziruhusiwi kisheria katika shughuli za biashara.
Aidha, baadhi ya AMCOS zimekuwa zikipunja wakulima kwa kuwasomea uzito usio sahihi wa mazao yao, hali inayowanyima haki ya malipo stahiki kulingana na uzito halisi wa mazao.
Mkanjabi ameeleza kuwa kuna baadhi ya vyama ambavyo havitumii mizani wakati wa kupokea mazao ya wakulima, bali husafirisha mazao hayo hadi kiwandani kwa ajili ya kupima, jambo linaloweza kusababisha upotevu wa haki za wakulima na kupunja ushuru wa chama husika
Vilevile, amesema kuna vyama vinavyoendelea kutumia mizani ambazo tayari zimebainika kuwa hazifanyi kazi kwa usahihi, jambo linalokiuka sheria na kuumiza wakulima.
Kufuatia changamoto hizo, katika musimu wa 2025/2026, Wakala wa Vipimo umejipanga kuendesha ukaguzi wa kushtukiza ili kubaini wale wanaochezea mizani na kutotii sheria ya Vipimo, Sura ya 340 pamoja na kanuni zake.
Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria hizo ili kuleta nidhamu na haki katika mizani zinazotumika katika ununuzi wa mazao ya wakulima.
Aidha, Mkanjabi amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na chama kikuu cha ushirika cha Mbinga (Mbifacu Ltd) katika kutoa mafunzo na semina kwa viongozi wa vyama vya ushirika, ili waweze kutambua wajibu wao katika kulinda uadilifu wakati wa matumizi ya mizani.
Amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kutoa taarifa mara moja pindi wanapobaini kuwa mizani haifanyi kazi kwa usahihi au imeharibika, ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
Social Plugin