Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI KUPATA MSAADA WA KISHERIA MKESHA WA MWENGE WA UHURU SONGEA

Waziri wa Katiba na Sheria pia Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mhe. Damas Ndumbaro akizungumza na wananchi wa Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea wakati wa Mwenge wa Uhuru ukiweka jiwe la msingi wa maegesho ya Magari

 Jiwe la msingi la maegesho ya magari Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea 

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, ametoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kupata huduma ya msaada wa kisheria, hususan wale wanaokumbwa na changamoto mbalimbali za kisheria. 

Ametoa wito huo leo Mei 14, 2025, wakati wa uzinduzi wa miradi iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru katika Manispaa ya Songea.

Mhe. Ndumbaro amesema huduma hiyo itatolewa katika viwanja vya Kata ya Ruvuma wakati wa mkesha wa Mwenge wa Uhuru, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC). 

Kampeni hiyo inalenga kuwafikia wananchi waliokosa uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria na kuwapatia msaada wa kitaalamu bure.

Ameeleza kuwa wananchi watakaofika kwenye eneo hilo watapata huduma za kisheria zinazohusu masuala ya ndoa, mirathi, madai, migogoro ya ardhi, pamoja na matatizo mengine ya kisheria yanayowakabili katika maisha yao ya kila siku. 

Huduma hizo zitatolewa na wanasheria waliobobea na watumishi wa serikali waliobobea katika masuala ya sheria.

Mhe. Ndumbaro amewahimiza wananchi wa Songea kutumia fursa hiyo adhimu ya mkesha wa Mwenge wa Uhuru kupata haki zao kwa njia halali na kuimarisha utawala wa sheria katika jamii. 

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka mkazo katika kuwahudumia wananchi kwa ukaribu na kwa vitendo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com