Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WA MSISIMA NA MNALAWI WAMEIPONGEZA SERIKALI KWA MRADI WA MAJI SAFI NA SALAMA

Tanki la Maji katika kijiji cha Msisima na Mnalawi halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma uliopo chini ya Mradi wa maji safi na salama vijijini (RUWASA)
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Ismail Ussi akizungumza na wananchi kabla ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo wa maji kijiji cha Msisima na Mnalawi Wilayani Namtumbo
Na Regina Ndumbaro Namtumbo-Ruvuma




Wananchi wa kata ya Msisima na Mnalawi, Wilaya ya Namtumbo, wameeleza furaha yao kubwa  kuuona mwenge wa Uhuru kwa mara ya kwanza tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961,baada ya mwenge wa uhuru kufika kijijini kwao. 

Wakiwa katika uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), wananchi hao wametoa shukrani zao kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea maendeleo na kuonesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia Watanzania wote bila ubaguzi.

Yasin Dauda na Zainabu Mjomba, wakazi wa vijiji hivyo, wameeleza kuwa mradi huo wa maji utasaidia kuondoa adha waliyozoea ya kutumia maji yasiyo salama, kupunguza umbali wa kutafuta maji na kuimarisha afya za familia zao. 

Wamesema kuwa huduma hii muhimu ni ya kihistoria na kielelezo cha utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita. 

Kwa heshima na kuthamini mchango wa Rais Samia, wameahidi kumpa kura zote katika uchaguzi mkuu ujao mwezi Oktoba, wamesisitiza kuwa hawatamwangusha kiongozi huyo aliyeonesha kuwajali kwa vitendo.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Namtumbo, Ndugu David Mkondya, Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 60. 

Mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 1.1, na unatarajiwa kunufaisha wakazi 481 kutoka vijiji viwili kwa kutumia chanzo cha maji kutoka Mto Msokambale. 

Mradi unahusisha ujenzi wa tanki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000, mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita saba, huku chanzo hicho kikiwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita milioni nne kwa siku ikilinganishwa na mahitaji ya lita 242,000 kwa siku. 

Mradi huo wa maji ulianza tarehe 17 Oktoba 2023 na unatarajiwa kukamilika tarehe 13 Juni 2025.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, amesisitiza kuwa mwenge wa uhuru umebeba ujumbe wa matumaini, amani, upendo na mshikamano kwa Watanzania. 

Ameeleza kuwa asilimia mia moja ya wakazi wa maeneo hayo watanufaika moja kwa moja na mradi huo wa maji. 

Pia amewahimiza wananchi kudumisha mshikamano, umoja na amani ili mradi huo uwe endelevu na kuleta mafanikio ya muda mrefu kwa jamii.

Kwa ujumla, ujio wa mwenge wa uhuru katika kata ya Msisima na Mnalawi umetajwa kuwa chachu ya maendeleo na ukombozi wa kweli kwa wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa muda mrefu. 

Serikali imeendelea kuonesha kwa vitendo kuwa dhamira ya kuwaletea Watanzania maendeleo si ya maneno bali ni ya vitendo, jambo ambalo limepongezwa kwa nguvu na wananchi wa maeneo hayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com