Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWENGE WA UHURU WAANZA KUMULIKA MIRADI MANISPAA YA SONGEA!

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mji Ngolo Malenya akimkabidhi  mwenge wa uhuru Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma

Kiongozi wa mbio za mwenge Ismail Ussi wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza katika hafla ya kukabidhi mwenge huo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mji kwenda Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma. 

Makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru yamefanyika leo tarehe 13 Mei 2025 katika shule ya msingi Likuyufusi, kata ya Lilambo, yakihusisha wilaya ya Mbinga Mji na Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma. 

Mbio za mwenge wa uhuru zinaongozwa kwa kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu”, ikiwa ni wito mahsusi kwa Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kidemokrasia kwa utulivu na mshikamano.

Katika makabidhiano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mji, Ngolo Malenya, amemkabidhi rasmi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile. 

Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wananchi na wakimbiza mwenge kitaifa, likiwa ni sehemu ya kuendeleza mshikamano wa kitaifa na uhamasishaji wa maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Ndg. Ismail Ussi, amewataka viongozi wa serikali kuendeleza juhudi zao katika kusimamia kazi za maendeleo na kuimarisha usalama katika kipindi chote cha uchaguzi. 

Amesisitiza kuwa Mheshimiwa Rais ana imani kubwa na viongozi waliopo katika ngazi zote na kwamba ni jukumu lao kuonyesha uaminifu huo kwa kuwatumikia wananchi kwa weledi, haki na usawa. 

Ameongeza kuwa wakimbiza mwenge wamefarijika na usimamizi mzuri walioukuta pamoja na ulinzi ulioboreshwa katika maeneo yote waliopitia.

Katika mbio hizo, Mwenge wa Uhuru umekimbizwa kwa jumla ya kilomita 66.6, ukipitia na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Jumla ya miradi nane yenye thamani ya shilingi bilioni 1.8 imetembelewa, kukaguliwa na kuzinduliwa, ikiwa ni ishara ya dhamira ya serikali kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli na endelevu. 

Wakimbiza mwenge wamesisitiza kuwa risala zote zilizopokelewa zitazingatiwa kwa ukamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kitaifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com