Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BANDARI CHANZO KINGINE CHA BIASHARA YA KABONI


Bandari zinaweza kuwa sehemu muhimu ya kuendeleza biashara ya kaboni kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira. 

Hayo yameelezwa na Bw. Ingvar M. Mathisen, Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Oslo, Norway, wakati wa ziara ya ujumbe wa Tanzania uliofika katika bandari hiyo hivi karibuni.

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mha. Masauni, ulitembelea bandari hiyo kwa lengo la kujifunza namna Bandari ya Oslo inavyohifadhi mazingira na kuzuia uzalishaji wa gesi joto.

Akizungumza, Mkurugenzi Mkuu wa Bandari hiyo, Bw. Mathisen, alieleza kuwa Bandari ya Oslo ni bandari mtambuka na haizalishi gesi joto. Bandari hiyo ni ya tatu kwa ukubwa duniani kwa kuwa na teknolojia janja ya bahari.

Lengo kuu la bandari hiyo ni kuhakikisha kuwa inapunguza gesi joto kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2030.

Serikali ya Norway imeazimia kufikia lengo hilo kwa kutumia teknolojia. Kuanzia mwaka 2018, Bandari ya Oslo imeacha kupokea na kuendesha meli zake kwa kutumia mafuta. Badala yake, meli zote — iwe za kusafirisha abiria, mizigo au za starehe — zinatumia umeme.

Kwa vyombo vyote ambavyo havitumii teknolojia hiyo, Bandari ya Oslo hutoza ada ya uzalishaji gesi joto — Emission Fees, ambayo inajumishwa katika mpango wa biashara ya kaboni.

Tanzania ni nchi yenye pwani ndefu ya Bahari ya Hindi upande wa mashariki, ikiwa na bandari kubwa za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, pamoja na bandari ndogo zinazohudumia maeneo ya Lindi, Kilwa Masoko, Mafia, Pangani na Kwale.

Bandari zote hizi hutumia vyombo vya usafirishaji. Hivyo, kwa kuwa na teknolojia ya kutambua kiwango cha gesi joto kinachozalishwa na kila chombo, mamlaka husika kwa kushirikiana na Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) zinaweza kushiriki katika biashara ya kaboni kwa kudai ada ya uzalishaji wa gesi joto.

Kupitia ziara hiyo, Tanzania imebainisha fursa mbalimbali za uhifadhi na usimamizi wa mazingira kupitia Uchumi wa Buluu na Biashara ya Kaboni.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com