Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWENGE WA UHURU WAZINDUA VISIMA TANDAHIMBA, WANANCHI WAPATA MAJI YA BOMBA KWA MARA YA KWANZA TANGU UHURU

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akikagua miundombinu ya mradi wa Kisima cha maji katika Kijiji cha Mivanga Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara kabla ya kuzindua mradi huo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akizindua mradi wa Kisima cha Maji katika Kijiji cha Mivanga Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara,kulia Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Mtwara Mhandisi Primy Damasi

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara Falaura Kikusa,akimuonyesha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi ,mchoro wa mradi wa Kisima cha maji uliotekelezwa katika Kijiji cha Mivanga.

Na Regina Ndumbaro-Tandahimba 

Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 umeweka historia katika Kijiji cha Mivanga, Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara baada ya kuzindua mradi wa uchimbaji wa visima vya maji, hatua iliyowapatia wakazi wa kijiji hicho huduma ya maji ya bomba kwa mara ya kwanza tangu Tanzania ipate Uhuru. 

Uzinduzi huo umefanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, ambaye alikagua na kuzindua rasmi kisima hicho akiwa ameongozana na viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba, Falaura Kikusa, amesema jumla ya Shilingi 452,500,000 zimetengwa kwa ajili ya kuchimba visima vitano katika vijiji vya Mivanga, Lyenje, Dinduma, Mchangani na Michenjele. 

Mradi huo ni sehemu ya programu ya uchimbaji wa visima 900 kote nchini, unaotekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani (force account), kwa kipindi cha miezi sita tangu Mei 2024, na unatarajiwa kukamilika Juni 2025 baada ya kuchelewa kutokana na changamoto mbalimbali.

Kwa mujibu wa Kikusa, hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya maji na usimikaji wa matanki ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 10,000 umekamilika katika vijiji viwili, huku usimikaji wa pampu na mfumo wa nishati ya jua ukifanyika katika vijiji vinne. 

Kisima cha Mivanga pekee kinazalisha lita 372,000 za maji kwa siku. 

Fedha za utekelezaji zinatokana na program ya Lipa kwa Matokeo, Mfuko wa Taifa wa Maji pamoja na michango ya wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, Katani Ahmed, ameishukuru serikali kwa kutatua tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, akisema kuwa mradi huo umepunguza changamoto kubwa iliyokuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo vijijini. 

Kwa upande wake, Ismail Ali Ussi amewataka wananchi kushirikiana na serikali kulinda miundombinu ya miradi hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija kwa jamii.

Asha Seleman, mkazi wa Kijiji cha Mivanga, amesema kabla ya mradi huo walilazimika kununua ndoo moja ya maji kwa Shilingi 1,000, jambo ambalo liliongeza gharama za maisha. 

Amesema sasa wameondokana na adha hiyo, na wana matumaini makubwa kuwa huduma hiyo itaboresha maisha yao kiuchumi na kiafya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com