Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

STAND UNITED KUIKABILI GEITA GOLD KATIKA MCHUANO WA MCHUJO WA KUPANDA LIGI KUU NBC ,DC MTATIRO AMELIPIA TIKETI ZOTE KUINGIA BUREE!

 

Wananchi wa Shinyanga na wapenzi wa soka nchini kwa ujumla wanatarajiwa kushuhudia mtanange wa kusisimua leo jioni katika Uwanja wa CCM Kambarage, ambapo timu ya Stand United itashuka dimbani kuvaana na Geita Gold katika mchezo wa marudiano (Leg 2) wa mchujo wa kupanda daraja kwenye Ligi Kuu NBC msimu wa 2024/25.

Mchezo huo, ambao utaanza saa 10:00 jioni, unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi kufuatia sare ya mabao 2-2 iliyopatikana katika mchezo wa kwanza. Kwa matokeo hayo, mshindi wa leo ataamua hatima ya kupanda Ligi Kuu, hivyo kufanya mchezo huu kuwa wa uamuzi mkubwa.

Katika taarifa kwa umma, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe.Wakili Julius Mtatiro, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia na kuisapoti timu ya Stand United. 

Amesema maandalizi yote yamekamilika na amefanikisha malipo ya tiketi zote ili kuhakikisha kuwa mashabiki wanapata fursa ya kuingia uwanjani bila kiingilio.

"Nawaalika nyote kwa moyo wa uzalendo kuja kuishangilia timu yetu. Kuketi uwanjani kutaanza saa 9:00 alasiri, na mchezo utaanza saa 10:00 jioni. Ni muhimu kufika mapema. Hakutakuwa na kiingilio – tiketi zote zimeshalipiwa", amesema Mtatiro.

Mchezo huu utakuwa wa aina yake, ukizingatia umuhimu wa kiushindani kati ya timu hizo mbili, na matarajio ya mkoa wa Shinyanga kuona Stand United ikirejea katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com