
Baada ya Yesu wa Tongaren, mwanamume mwingine kutoka magharibi mwa Kenya, mara hii kutoka kaunti ya Kakamega nchini Kenya, amejitokeza kudai kuwa yeye ndiye ‘Mungu wa tatu’.
Alfred Ndeta, ambaye anaishi eneo la Shibuli katika kaunti ndogo ya Lurambi, pia anadai kuwa yeye ni babaake Yesu.
Kulingana na Ndeta, alipokea ufunuo mwaka wa 1987 uliomwagiza ahamie kijijini kwake cha sasa, anachodai kuwa ni mbinguni.
Mwanaume huyu wa makamo anayedai hajawahi kuoga na haendi haja kubwa amesema alimsikia Roho Mtakatifu akizungumza naye akiwa Nairobi.
Ni baada ya tukio hilo ndipo alihamia kijijini, mahali ambapo amekuwa akiishi kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

"Nilijipata tu nikiwa Nairobi. Sijui nilikotoka, na ndipo nikasikia sauti ya ajabu kutoka kwa mtu aliyedai kuwa Roho Mtakatifu wakati nilikuwa usingizini. Aliniamuru nisafiri kutoka Nairobi hadi mbinguni (Shibuli) kwa mwili wa aina ya duma ndipo nikaanza kujenga mbingu yangu mnamo Machi 1987," Ndeta aliambia chombo cha habari cha TUKO.co.ke katika mahojiano ya kipekee.
Je, Alfred Ndeta ameoa?
Mungu huyu anayejiita kwa jina lake mwenyewe alisema hajawahi oa kwa sababu anaamini kuchanganya mapenzi na imani zake kungezuia kazi yake na kuathiri uwezo wake wa kutoa mapepo ndani ya wanadamu.
"Nilikuwa na mtoto, lakini sina mke. Siwezi changanya kazi yangu na wanawake kwa sababu wanaweza kuzuia huduma yangu kwa wanadamu," alisema.
Ndeta, ambaye ana nywele ndefu kama za Rastafarian, anadai amefanya mambo mengi yanayothibitisha kuwa yeye ni ‘mungu wa tatu’.
Inasemekana aliwahi kuamuru watu wa kijiji wahame kutoka walikokuwa wakiishi, agizo lililoheshimiwa baada ya kuchinja kondoo watatu kando ya mto.
Katika boma lake analodai kuwa ni mbinguni, Ndeta amegawanya nyumba yake katika sehemu tatu – moja ni ya "kiti cha enzi", nyingine ni kwa ajili ya Roho Mtakatifu na ya tatu ni jehanamu.
"Hapa mbinguni nina sehemu tatu; moja ni pale nilipoweka kiti cha ufalme wangu, nyingine kama unavyoona kuna moto wa kudumu unaotumika kuponya magonjwa, sanamu ya ng’ombe ambayo hufichua wanaopinga mapenzi yangu na wenye nia mbaya. Nina pia chumba cha Roho Mtakatifu. Hana mikono kwa sababu huwa anaruka mara kwa mara," Ndeta alieleza.
Ingawa Ndeta anaamini yeye ni Mungu, wakazi wa eneo la Shibuli wanasema yeye si mtu wa kawaida.
Baadhi yao wanadai ana uwezo wa kutoa mapepo kwa mtu, huku wengine wakishuhudia kuwa wamewahi kuona akiponya wagonjwa.
Mwanaume wa Bungoma anayejidai kuwa yeye ni Yesu Awali, tuliripoti kuwa mwanaume mwingine aliibuka akidai kuwa yeye ni mwana wa Mungu.
Tofauti na Yehova Wanyonyi na Yesu wa Tongareni, Mwalimu Yesu alidai kuwa yeye ndiye Yesu Kristo wa kamili.
Pia alidai kuwa ndiye Masiha wa kweli ambaye Mungu alimtuma duniani kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu
Social Plugin