Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson akizungumza na wakazi wa jiji la Mbeya wakati wa Mafunzo ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (Samia Legal Aid)Jijini Mbeya
Wakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Haruna Matata akizungumza na wakazi wa Jiji la Mbeya wakati wa kutoa Mafunzo hayo ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia Legal Aid
****
Na Regina Ndumbaro-Mbeya
Zaidi ya viongozi 4,000 wa ngazi ya Serikali za Mitaa kutoka kata saba za Halmashauri ya Jiji la Mbeya wamepatiwa mafunzo ya utawala bora, elimu ya uraia na mbinu mbadala za kutatua migogoro, ikiwemo ukatili wa kijinsia.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, yenye lengo la kuwawezesha viongozi kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
Akizungumza leo Mei 22, 2025, wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Mbeya, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amewahimiza viongozi hao kutumia elimu waliyoipata kwa vitendo ili kutatua kero za wananchi kwa njia za amani na zinazozingatia haki.
Amesisitiza kuwa wananchi wanahitaji viongozi wanaojua namna ya kusikiliza, kuelewa na kutatua matatizo yao kwa ufanisi.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku ya pili mfululizo na yamejikita katika kuwawezesha viongozi kuimarisha misingi ya utawala bora, kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi na kuimarisha mahusiano kati ya viongozi na wananchi.
Aidha, wamefundishwa namna ya kushughulikia migogoro kwa kutumia njia za maridhiano badala ya kutumia nguvu au kukimbilia vyombo vya sheria mara moja.
Dkt. Tulia pia ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii na kisiasa kwa kuwa na uelewa wa haki na wajibu wao kama raia.
Amesema kuwa maendeleo ya taifa yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya viongozi na wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali.
Kupitia kampeni hii, serikali inalenga kueneza elimu ya kisheria kwa jamii nzima, huku viongozi wakipewa jukumu la kuwa daraja la mawasiliano kati ya serikali na wananchi.
Mafunzo hayo yamepokelewa kwa shukrani na matumaini makubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika usimamizi wa maendeleo na ustawi wa wananchi wa Jiji la Mbeya.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson akiwa katika Picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi waliojitokeza katika Mafunzo ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia Legal Aid Jijini Mbeya

Baadhi ya Wananchi na Wakazi wa Jiji la Mbeya wakiwa katika Mafunzo ya Elimu ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia Legal Aid
Social Plugin