Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU RUVUMA YAOKOA MILIONI 9 SONGEA, YACHANGIA ONGEZEKO LA MAPATO


Naibu Mkuu wa TAKUKURU Ruvuma, Janeth Haule

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ruvuma imetoa taarifa ya mafanikio ya utendaji kazi wake kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025, ikionyesha jinsi ilivyosaidia kuokoa shilingi 9,205,158.44 ambazo zilikuwa zimekusanywa na mawakala wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kutoka vyanzo mbalimbali lakini hazikuwasilishwa benki kama taratibu zinavyoelekeza. 

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Ruvuma, Janeth Haule, ameeleza  hayo leo Mei  30, 2025 kuwa fedha hizo zilifuatiliwa na hatimaye kuwasilishwa benki kupitia mifumo ya kielektroniki.

Aidha, TAKUKURU imeeleza kuwa ufuatiliaji huo umechochea ongezeko la mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea hususan kwenye Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Biashara, Ardhi na Maliasili. 

Mapato hayo yameongezeka kutoka asilimia 50 hadi kufikia asilimia 102 ya makusanyo kupitia mifumo ya kielektroniki, hatua inayothibitisha mafanikio ya udhibiti na usimamizi madhubuti wa fedha za umma.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU imebaini na kutoa marekebisho ya mapungufu yaliyokuwepo katika utekelezaji wa miradi mitatu mikubwa inayogharimu jumla ya shilingi 29,917,135,361.43. Miradi hiyo inahusisha sekta za miundombinu, kilimo na fedha, ambapo TAKUKURU imeingilia kati kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia thamani halisi ya fedha.

Janeth Haule amesisitiza kuwa TAKUKURU itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha fedha za umma zinasimamiwa ipasavyo na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa ili kuleta manufaa kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com