Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Alexius Kagunze na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Ramadhani Masumbuko (kulia) wakiwa kwenye kikao Mei 6,2025
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga limekutana katika kikao cha robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo pamoja na kuwasilisha taarifa za maendeleo ya kata zao, wametoa mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuimarisha huduma za jamii, hususan kwenye sekta ya miundombinu, elimu na mazingira bora ya utendaji kazi.
Katika kikao hicho kilichofanyika leo Mei 6,2025, madiwani walieleza umuhimu wa kuendeleza jitihada za kuboresha barabara za ndani, kuongeza matundu ya vyoo katika baadhi ya shule za msingi, na kuhakikisha upatikanaji wa ofisi za watendaji katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Wamesema hoja hizo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara kutoka kwa wananchi, na wanaamini kupitia ushirikiano na menejimenti ya halmashauri, changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Diwani wa Kata ya Kizumbi, Mheshimiwa Reuben Kitinya, ameeleza kuwa baadhi ya maeneo yanahitaji maboresho zaidi ya barabara na miundombinu ya shule ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Manispaa.
“Lengo letu ni kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira salama na bora, huku wananchi wakiweza kufikia huduma muhimu kwa urahisi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Alexius Kagunze, ameeleza kuwa halmashauri tayari imetenga Shilingi milioni 61 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa barabara, na kwamba mpango wa utekelezaji utaanza mara tu msimu wa mvua utakapoisha.
“Tunaendelea na maandalizi kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo. Barabara zote zitalimwa kulingana na bajeti iliyotengwa,” amesema Kagunze.
Katika shule ya msingi Lyandu na Bugayambelele, ambapo vyoo vinahitaji kuongezwa, Mkurugenzi amesema kuwa tayari taarifa zimepokelewa na hatua za kupanga ujenzi wa vyoo hivyo zinaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Ramadhani Masumbuko, amesisitiza umuhimu wa kushughulikia maeneo ya shule ambayo yamezungukwa na makazi ya watu kwa lengo la kuzuia migogoro ya ardhi.
Pia, ametoa maelekezo maalum kwa Afisa Elimu Sekondari kufuatilia hali ya utoro wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Chibe ambapo kiwango cha utoro kimeripotiwa kufikia asilimia 24.
“Nimeelekeza watendaji wa kata, uongozi wa shule na Afisa Elimu kushirikiana kwa karibu kufuatilia suala hilo ili kubaini sababu na kuchukua hatua stahiki kwa manufaa ya wanafunzi na maendeleo ya elimu kwa ujumla,” amesema Meya Masumbuko.
Social Plugin