
Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, asasi mbalimbali za kiraia Zanzibar zimehimiza wanawake kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi ndani ya vyama vya siasa.
Asasi hizo zikiwemo TAMWA ZNZ, JUWAUZA, ZAFELA na PEGAO — zinasema ushiriki wa wanawake katika uongozi ni muhimu kwa kuleta usawa wa kijinsia na kuhakikisha maamuzi yanayofanywa yanazingatia mahitaji ya jamii nzima.
Kwa sasa, vyama vya siasa vimeanza kutoa fomu za kugombea nafasi mbalimbali kama udiwani, uwakilishi, ubunge na hata urais. Asasi hizi zinawataka wanawake wote wenye sifa kuchangamkia fursa hii muhimu kwa kuchukua na kujaza fomu hizo mapema.
Kupitia Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Zanzibar (SWIL), zaidi ya wanawake 200 kutoka Unguja na Pemba tayari wamepatiwa mafunzo ya uongozi, kuwajengea uwezo wa kujiamini na kushiriki kikamilifu katika nafasi za maamuzi.
Hata hivyo, bado changamoto ipo. Ripoti ya uchaguzi wa 2020 iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar inaonesha kuwa kati ya wagombea 601 waliotia nia, wanawake walikuwa 135 pekee, sawa na asilimia 22.4. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa bado wanawake hawajatumia ipasavyo haki yao ya kushiriki uongozi wa taifa.
Katika kuhakikisha uchaguzi wa 2025 unakuwa wa haki na uwazi, wanawake pia wamehimizwa kuepuka na kuripoti vitendo vyovyote vya rushwa, wakikumbushwa kuhusu sheria mpya ya Zanzibar ya Kuzuia Rushwa na Uhalifu wa Kiuchumi Na. 5 ya mwaka 2023, ambayo inatoa adhabu kali kwa yeyote atakayehusika na rushwa.
Kwa pamoja, asasi hizi zimeahidi kuendelea kutoa msaada, elimu na hamasa kwa wanawake wote, wakisisitiza kuwa usawa wa kijinsia katika uongozi ni msingi wa demokrasia imara na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Wito wao uko wazi:
"Wanawake, changamkieni fursa ya uongozi, simameni, shiriki, na leteni mabadiliko ndani ya jamii zenu!"
Social Plugin