
Na Hadija Bagasha - Korogwe
Wananchi wa Halmashauri ya Korogwe mji wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwafikishia huduma ya msaada wa kisheria ambayo wamepata fursa ya kutatuliwa migogoro yao iliyokuwa ikiwakabili kwa kipindi kirefu bila kupatiwa ufumbuzi.
Wananchi hao wamesema wamehangaika kwa miaka mingi kutafuta haki zao bila mafanikio yeyote lakini kupitia kampeni hiyo wamefanikiwa kushughulikiwa changamoto zinazowakabili bila gharama yeyote jambo lililoteta mafanikio makubwa kwao.
Wakizungumza na kituo hiki wananchi hao wamesema kampeni hiyo imefika wakati muafaka na imewasadia kujua haki zao za msingi ambazo walikuwa hawazitambui hapo awali na kwamba huduma hiyo imewafikia ipasavyo hususani wananchi wanyonge waliodhulumiwa haki zao.
"Tunamshukuru sana mtetezi wa wanyonge mama yetu Samia Suluhu Hasaan Kwa kutuletea timu hii ambayo jnatafuta haki za watu za kisheria kwa mfano sisi kero yetu kubwa iliyokuwa ikitusumbua tulidhulumiwa eneo letu lakini kupitia hii kampeni tumeweza kupata elimu na ushauri lakini pia hata yule aliyedhulumu eneo letu ameitwa na kesho atakutana na hawa wanasheria, "alisema Bi Aisha mkazi wa Lwengera Darajani.
Gerald Kajiru Mkulima na mkazi wa Lwengera Darajani amesema walikuwa wanakabiliwa na kero ya muda mrefu ya N'gombe kuingia mashambani na kula mazao yao jambo ambalo limewaathiri kiuchumi na kwamba kupitia kampeni hiyo wameweza kutatuliwa kadhia hiyo.
"Sisi kero yetu kubwa ambayo ilikuwa ikitusumbua ni N'gombe wafugaji tumehangaika nao kwa muda mrefu zaidi ya miaka mungi mno tumekwenda kwenye ngazi nyingi lakini imeshindikana lakini tunashukuru kwa kuja hii kampeni ya mama Samia inakwenda kutatua jambo letu kwakuwa tulijipanga kuingia porini na silaha tukawawinde ili tukabiliane nao kama damu imwagike, "alisisitiza Gerald.
Wakili msomi George Banoba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria akiwa wilayani Korogwe kwajili ya kutekeleza kampeni hiyo amesema elimu waliyoitoa ni pamoja na elimu ya ndoa, mirathi, ardhi, masuala ya ukatili wa watoto, ukatili wa kijinsia, matunzo ya watoto ambapo wananchi wameonyesha mwitikio mkubwa huku akielezea changamoto zilizokuwa zinawakabili wananchi hao.
"Changamoto kubwa ambayo tumeikuta hapa ni mgogoro mkubwa wa ardhi ambako inaonekana watu wengi waligawiwa eneo na maeneo ya makazi katika eneo lililokuwa linamilikiwa na Korogwe Estate lakini baadae inaonekana hilo eneo limekuja kumilikiwa na watu wengine lakini migogoro hiyo tumeichukua kwajili ya kuifanyia uchunguzi wa kina ili iweze kupata suluhisho, "alibainisha Wakili Banoba kutoka Wizara ya Katiba na sheria.
Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia ipo Wilayani Korogwe kwa muda wa siku 9 pia imeambatana na kutoa elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia ya ubakaji na ulawiti ambayo wamekuwa wakifanyiwa watoto, na kuzifikia shule za sekondari na msingi katika Halmashauri ya Korogwe mji ikiwemo shule ya wasichana ya Korogwe Girls, Old Korogwe, na Shemsanga huku shule ya msingi ikiwa Kitopeni, Lwengera Darajani, pamoja na Lwengera Relini.
Social Plugin