
Mwenyekiti wa Kijiji cha Cheketu Kata ya Somanga Hashimu Changajua akizungumza na Wananchi wa Kijiji hicho cha Cheketu kuhusu Sheria walizoziweka kati ya Wakulima na Wafugaji

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Cheketu Kata ya Somanga Wilayani Kilwa


Na Regina Ndumbaro Kilwa-Lindi.
Wakulima wa kitongoji cha Cheketu, kata ya Somanga wilayani Kilwa, wameonesha kutoridhishwa na vitendo vya wafugaji wanaoingiza mifugo yao kiholela kwenye maeneo ya wakulima, hali inayosababisha migogoro ya mara kwa mara.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliolenga kutoa elimu kuhusu sheria ndogo za halmashauri ya Kilwa kuhusu mahusiano ya wakulima na wafugaji, wakulima hao wameitaka serikali kuchukua hatua madhubuti kudhibiti hali hiyo.
Ali Mzungu, mkulima kutoka kitongoji hicho, amesema kata ya Somanga haijatenga maeneo rasmi kwa ajili ya wafugaji, jambo linalowafanya wafugaji kununua mashamba na kuingiza mifugo kwa idadi kubwa, bila kuzingatia matumizi ya ardhi yaliyopo.
Ametoa wito kwa serikali kuu kuielekeza serikali ya kijiji cha Somanga kutenga maeneo rasmi na kuweka mipaka kwa alama maalum zitakazoonesha utengano kati ya maeneo ya wakulima na wafugaji.
Kwa upande wake, Mwenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Somanga, Saidi Japhet, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kwa kutunga sheria ndogo zinazolenga kutatua changamoto za muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji.
Hata hivyo, amesisitiza haja ya serikali kuwa wazi kuhusu uhalali wa matumizi ya ardhi na kuhakikisha kuwa kila kundi linatambua mipaka ya maeneo yao ili kulinda amani ya jamii.
Awali, Mwenyekiti wa kitongoji cha Cheketu, Hashimu Changajua, amewaeleza wakulima kuhusu sheria hizo ndogo, akisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuzifahamu ili kutambua haki na wajibu wao.
Ameeleza kuwa elimu hiyo itasaidia kuimarisha uelewa wa pamoja na kuondoa migogoro isiyo ya lazima baina ya wakulima na wafugaji.
Social Plugin