Tanzania imeendelea kuonesha dhamira yake thabiti katika kuendeleza maendeleo na haki za jamii kupitia ushiriki wake katika Mkutano wa 150 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaofanyika mjini Kashkenti, Uzbekistani kuanzia tarehe 5 hadi 9 Aprili 2025.
Mkutano huu unaojadili kwa kina nafasi ya Mabunge katika kupigania maendeleo na haki za jamii (Social Development and Justice), umezikutanisha nchi wanachama kujadili njia bora za kuimarisha uwajibikaji wa serikali kwa maslahi ya wananchi.
Katika mkutano huo, Tanzania imewakilishwa na msafara wa Wabunge ukiongozwa na Mhe. Joseph Kizito Mhagama, ambaye alipata fursa ya kulielezea Bunge la Tanzania na mchango wake katika kuisimamia Serikali ili kuhakikisha kuwa haki za kijamii na maendeleo endelevu vinafikiwa.
Mhe. Mhagama ameeleza namna ambavyo Bunge la Tanzania limekuwa likihimiza uwajibikaji, kutunga sheria zinazolinda haki za jamii, na kufuatilia utekelezaji wa sera mbalimbali zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.
Kupitia hotuba yake, Mhe. Mhagama amegusia hatua mahususi zilizochukuliwa na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za afya, elimu, maji safi na usawa wa kijinsia, ambazo zote zinaakisi dhamira ya Taifa katika kulinda haki za kijamii.
Pia ameeleza kuhusu jitihada za Bunge katika kupokea na kuchambua taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kama mojawapo ya njia ya kuhakikisha uwajibikaji wa matumizi ya fedha za umma.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu umeimarisha nafasi yake kimataifa na kutoa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na nchi nyingine kuhusu masuala ya kijamii.
Social Plugin