Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MACHA: SERIKALI YA MKOA WA SHINYANGA KUJIPANGA KUIMARISHA VYAMA VYA MSINGI VYA USHIRIKA AMCOS




NA NEEMA NKUMBI - KAHAMA


Serikali ya Mkoa wa Shinyanga imeweka mkakati mahsusi wa kuviimarisha vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS), ikiwa ni juhudi za kuhakikisha vyama hivyo vinakuwa na tija sawa na ile inayoshuhudiwa kwenye vyama vikuu vya ushirika vinavyofanya kazi kwa mafanikio makubwa mkoani humo.


Akizungumza katika Jukwaa la Ushirika lililofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, amesisitiza kuwa ipo haja ya kuviwezesha vyama vya msingi kuwa imara, endelevu na vyenye mchango halisi kwa wanachama wake na kwa uchumi wa mkoa.


Mhe. Macha amewataka viongozi na wanachama wa vyama vya SHIRECU na KACU kusimamia kwa uadilifu rasilimali za wakulima, akieleza kuwa usimamizi bora wa mali za ushirika ndio msingi wa mafanikio. Hatua hiyo inalenga kuifanya sekta ya ushirika kuchangia kikamilifu pato la Mkoa na Taifa.


Katika mkutano huo, RC Macha alitoa agizo kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Bw. Emmanuel Nyambi, kuitisha kikao maalum kitakachowajumuisha viongozi wa vyama vya msingi visivyopewa kipaumbele kama vile vya Wafugaji na Wachimbaji wa Madini, Lengo la kikao hicho ni kujadili changamoto, kutafuta suluhu na kubuni mbinu mpya za kuboresha utekelezaji wa majukumu ya vyama hivyo.


“Nakuagiza Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Shinyanga ndugu Nyambi, uandae kikao hicho ili tuweze kujadili changamoto na kuhakikisha kuwa utekelezaji wa majukumu unaendana na matokeo chanya kwa jamii na uchumi wa Mkoa kwa ujumla,” amesema RC Macha.


Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Kakozi Ibrahim, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa AMCOS kujitathmini kuhusu utendaji na uwajibikaji wao kwa wanachama huku akieleza kuwa mafanikio au kushindwa kwa chama yanategemea moja kwa moja uwezo na uadilifu wa viongozi wake, hivyo ni muhimu kuwa na viongozi wenye maono, ufanisi na uwazi.


Naye Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emanuel Cherehani, ametoa rai kwa vyama vya ushirika kuhakikisha vinatayarisha taarifa sahihi za fedha na matumizi kulingana na viwango vya kiuhasibu pia kuzingatia kanuni na maadili ya ushirika ili kuhakikisha vyama vinadumu na kuwa na tija.


Kaulimbiu ya Mwaka huu: “Ushirika Hujenga Ulimwengu Uliyo Bora.”





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com