Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA WILAYA TUNDURU AONGOZA KIKAO NA WAFANYABIASHARA, AHIMIZA UMOJA NA USHIRIKIANO



Na Regina Ndumbaro Tunduru .

Mkuu wa Wilaya ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Mhe. Saimon Chacha, amekutana na wafanyabiashara wa halmashauri hiyo kwa lengo la kushukuru kwa mafanikio yaliyopatikana na kuhimiza mshikamano wa pamoja katika maendeleo ya wilaya.

Akizungumza katika kikao hicho na wadau, Mhe. Chacha ameeleza kuwa kila mmoja ana nafasi na mchango wake katika jamii bila kujali kada, chama au asili yake, hivyo ni muhimu kushirikiana kama wana Tunduru kwa ajili ya ustawi wa pamoja.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa ni muhimu kujenga umoja baina ya wafanyabiashara, watumishi wa serikali na wananchi kwa ujumla.

Amesema kuwa bila kushirikiana, jamii inaweza kugawanyika na kila mtu akaishi kivyake hali ambayo inahatarisha maendeleo ya pamoja. “Imani yangu ni kuwa tukishirikiana kwa upendo, tutaondoa malalamiko na migogoro isiyo ya lazima,” amesema.

Mhe. Chacha Ameeleza kuwa kuna baadhi ya watu hujihisi kutengwa au kuona chuki kutoka kwa wenyeji hasa pale wanapokuja kutoka maeneo mengine.

Amewataka wananchi kuachana na chuki, kwani kutokujituma na kuona wageni wakifanikiwa kunaweza kuleta uhasama usio wa lazima.

Amehimiza mshikamano, upendo, kusaidiana na kuwa na ushirikiano mzuri baina ya wote, hasa wafanyabiashara na watumishi wa serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Ephraim Bwilo, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuwashirikisha katika majadiliano ya kuimarisha mshikamano baina ya wananchi wenyeji na wageni.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inaonyesha namna viongozi wanavyowathamini wafanyabiashara na mchango wao katika maendeleo ya wilaya.

Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mikutano kama hiyo kwa ajili ya kujadili changamoto na mafanikio kwa pamoja.

Aidha, Bwilo amewahimiza wananchi wa Tunduru kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao, akisema ni haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowataka.

Ametoa wito kwa viongozi kuendeleza ushirikiano na wafanyabiashara kwa ajili ya maendeleo ya Tunduru, huku akiahidi kuwa wafanyabiashara wataendelea kushirikiana kikamilifu na serikali katika kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com