Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BURUTE SACCOS KAGERA YAFANIKIWA KUKUSANYA AMANA ZA MILIONI 802


Na Lydia Lugakila, Bukoba

Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo kwa Watumishi wa Umma kwa Wilaya za Bukoba na Misenyi mkoani Kagera Burute Saccos Limited kimeeleza kufanikiwa pakubwa katika kukusanya Amana zenye thamani ya shilingi milioni 802,866, 173 kutoka wanachama 37 ambapo kati yao wanachama 11 bado kwenye utumishi yaani bado hawajastaafu.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja Burute Saccos Limited Mkoa wa Kagera Godian Stephen kwa niaba ya mwenyekiti wa bodi ya Burute katika mafunzo kwa wanachma wastaafu pamoja na wawekezaji wa amana za muda yaliyofanyika katika ukumbi wa St.Theresa uliopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.

Kupitia Muhtasari aliousoma mbele ya wanachama hao na Mgeni rasmi, Meneja huyo amesema kuwa wakati wanaanza zoezi la kutoa elimu ya fedha chama nilikuwa na Amana zenye thamani ya shilingi milioni 208,413,625 ambazo zilikusanywa kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano ambazo zilikuwa zikipewa faida au riba ya asilimia 7 lakini hadi sasa wamepiga hatua kubwa.

"Tumefanikiwa kukusanya Amana zenye thamani ya shilingi milioni 802, 866, 173 fedha hizo zimewekwa kwenye chama kwa mkataba wa kipindi cha muda maalum kuanzia miezi mitatu hadi mwaka mmjoa alisema Godian".

Ameongeza kuwa kutokana na uwekezaji huo chama kimetoa faida juu ya Amana kiasi cha milioni 50,282,387 kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2024, ambapo faida hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa wawekezaji kwani wanaruhusiwa kuichukua kila baada ya miezi mitatu mitatu.

Chama hicho kimeendesha mafunzo juu ya elimu ya fedha kwa wanachama wastaafu pamoja na wawekezaji wa amana za muda maalum ili kuwajengea kesho iliyo nzuri ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali wanapopata pesa sambamba na kutengeneza kipato endelevu kupitia uwekezaji.

Godian amesema kuwa zoezi hilo la kutoa elimu linafanyika kwa mara ya tatu baada ya ya kufanyika kwa miaka miwili iliyopita mfululizo ambapo pia mafunzo hayo husaidia kuwakutanisha pamoja wastaafu ambapo hujadili mambo mbali mbali yanayohusu maisha kabla na baada ya kustaafu .

Aidha ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya kanuni ya utoaji wa mafao kwa wastaafu wa kazi za umma kubadilika mwaka mnamo mwaka 2023 bodi ilibuni njia bora ya kutoa elimu kwa wanachama wastaafu na wanaotarajia kustaafu kuhusian na maisha baada ya kustaafu na namna bora ya utunzaji wa fedha.

Meneja huyo amesema Burute imezidi kufanya vizuri pamoja na kuwa na mipango mizuri huku akizitaja changamoto mbali mbali zilizojitokeza katika uendeshaji wa huduma hiyo kuwa ni pamoja baadhi ya wawekezaji kutoendelea na uwekezaji baada ya kumaliza mikataba yao, uwepo wa watumishi wanachama wastaafu wasiowekeza katika chama badala yake hupeleka fedha hizo katika taasisi nyingine.

Pamoja na mambo mengine amesema kuwa faida ya asilimia 10 ambayo chama kinatoa kutokana na wawekezaji, bodi inakusudia kuanzisha mradi wa pamoja ambao utatokana na wawekezaji hao kununua hisa kutokana na faida inayopatikana ama kununua kutokana na fedha waliyowekeza jambo ambalo litatengeneza kipato endelevu kwa wawekezaji.

Akifungua Mafunzo hayo mgeni rasmi ambaye ni Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Kagera, Enikia Bisanda ametumia fursa hiyo kuwaomba wanachama hao waliostaafu na ambao bado hawajastaafu kutumia elimu ya fedha vizuri ili maisha ya kustaafu au kabla ya kustaafu yawe rahisi kuliko kupokea fedha na kushindwa kujua la kufanya.

"Nawaomba mjitahidi kuweka mpango wa kustaafu ikiwemo kufanya biashara mliyo na uzoefu nayo, wekeni pesa zenu Burute kwani ni sehemu sahihi zitakuwa na ulinzi salama tumieni Burute Saccos ili muepuke presha ya uzee" alisema Bisanda.

Amewahimiza wanachama hao kukipenda chama hicho na kuendelea kuwekeza ili kujiinua kiuchumi kwa malengo ya baadae huku wakiitumia elimu ya fedha ili kufanikiwa zaidi.

Mrajis huyo ameishukuru bodi ya Burute kwa juhudi kubwa kwani kwa Kagera wanajivunia makubwa yaliyotokana na chama hicho.

Aidha Bisanda amewasisitiza kutunza pesa zao sehemu sahihi ili kutengeneza maisha ya baadae bila kupata miangaiko inayoweza kuwaletea msongo wa mawazo baada ya kustaafu huku akihitaji wawe na nidhamu katika fedha ili kufanikisha malengo kusudiwa

Mafunzo hayo yameenda sambamba na kutoa tuzo kwa watu 20 waliowekeza vizuri Amana za muda maalum ambapo pia limefanyika bonanza kubwa lililohusisha michezombali mbali ikiwemo kukimbia kwenye gunia, kukimbia na yai, kumenya ndizi na kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com