Wananchi wa kitongoji cha Bugwandege, kilichopo katika Kijiji cha Uzogore, Kata ya Ibadakuli, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, wameiomba serikali kusogeza huduma ya afya karibu nao kutokana na zahanati inayohudumia eneo hilo kuwa na zaidi ya miaka 25 bila kukamilika.
Zahanati hiyo ilianza kujengwa mwaka 1998 kwa juhudi za wanakijiji waliokuwa wakijitolea.
Hata hivyo, baada ya kujenga lenta, kazi ilikwama na mpaka leo haijakamilika.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Ngasa Katambi, alisema kuwa licha ya changamoto hiyo, zahanati hiyo inaweza kuhudumia zaidi ya wananchi 1000.
Aliongeza kuwa atashirikiana na Diwani wa Kata, na kama jambo hilo litakuwa gumu, atajitahidi kulifikisha kwa Mbunge ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri za afya.
Wakazi wa Kitongoji cha Bugwandege, kama Bisiye Magumba, wamesema kuwa changamoto wanayokutana nayo ni kubwa, hasa kwa wanawake, kwani baadhi yao wanajifungulia njiani kutokana na umbali mrefu wa huduma ya afya.
Hii inahatarisha maisha ya mama na mtoto. Peter John, mkazi mwingine, alisema kuwa wanatoka Bugwandege hadi Ibadakuli au Kolandoto kwa ajili ya huduma za afya, ambapo umbali ni kilomita 8 na gharama ya usafiri ni shilingi 4000 kwa pikipiki.
Gharama hii ni kubwa kwa kipato cha kawaida, hivyo wanajikuta wakitembea kwa miguu.
Zengu Magina, mkazi mwingine, alieleza kwa uchungu kuwa mke wake alishawahi kujifungulia njiani kutokana na umbali wa zahanati. Alisema kuwa zahanati hiyo imekuwa ni ahadi za kisiasa kutoka kwa wagombea, lakini baada ya kushika madaraka, ahadi hizo hazitekelezwi.
Naye, Mkuu wa Divisheni ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Elisha Robert, alisema kuwa kuna maboma mengi ya zahanati ambayo hayajakamilika, na zahanati ya Uzogore ni miongoni mwa maeneo yaliyo kwenye bajeti ya ukamilishaji kwa mwaka ujao wa fedha, 2025/2026.
Aliongeza kuwa kwa mwaka huu bajeti ya ukamilikaji wa zahanati hiyo haipo vizuri.
Diwani wa Kata ya Ibadakuli, Msabila Malale, alikiri kuwa zahanati hiyo ina muda mrefu bila kumalizika, lakini hakuwa na uhakika kama suala hili lilitumika kama sera ya kisiasa kwa wagombea. Hata hivyo, alithibitisha kuwa ukamilikaji wa zahanati hiyo umejumuishwa kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha na itakamilishwa.
Katika hali hii, wananchi wa Bugwandege wanahitaji msaada wa haraka ili kupata huduma bora za afya kwa ustawi wao na wa familia zao.
Social Plugin