Na Hadija Bagasha - Tanga
RAIS Samia Suluhu Hassan amepigilia msumari uamuzi wa wafanyabiashara wa mafuta kununua mafuta kwenye bohari ya mafuta ya GBP iliyopo Mkoani Tanga badala ya kwenda Bandari ya Dar es Salaam mahala ambapo wanasababisha msongamano mkubwa.
Siku ya saba na ya mwisho ya ziara ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika bohari ya mafuta ya GBP jijini Tanga mahali ambapo Rais amepigilia msumari uamuzi wake wa awali wa kuwataka wafanyabiashara wa kanda ya kaskazini kununulia mafuta Tanga badala ya kwenda Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa nishati safi wa LPG kwenye bohari ya mafuta ya GPB iliyopo jijini Tanga ,Rais Samia Suluhu Hassan amesema mpango huo utasaidia kupunguza foleni katika Bandari ya Dar Es Salaam.
"Nataka niseme wakati naangalia mradi huu wa LPG nimeona pia dhamira yenu ya kuwekeza katika vituo vya kujaza gesi GBP katika kila Mkoa huu ni uwekezaji mkubwa sana na nataka niwahakikishie kuwa serikali inaunga mkono jitihada hizi, alisisitiza Rais Dkt. Samia.
Pia Rais Dkt Samia ameiomba kampuni ya GBP kupitia mkurugenzi mkuu na mmiliki wake Badar Soud kutekeleza mpango wao wa kuwekeza shilingi bilioni 50 katika mradi wa vituo vya kujaza mitungi ya gesi katika kila Mkoa Nchini.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema mradi huo amesema sera nzuri za uwekezaji zimwekuwa zikiwavutia wawekezaji na hivyo kuwafanya waone umuhimu wa kuwekeza nchini na hatimaye kusaidia kukabiliana na changamoto ya ajira mkoa huo.
Naye Mkurugenzi wa GBP Badar Soud amesema mradi huo amempongeza Mh Rais Samia Suluhu Hasaani kwa kuleta mabadiliko kwenye matumizi ya nishati safi kwa lengo la kupunguza maradhi yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
Mradi huo upo kwenye mpango wa serikali wa kuwataka watanzania kuanza kutumia nishati safi ya kupikia badala ya matumizi ya mkaa na kuni ambayo yanachangia kwenye uharibifu wa mazingira.
Baadhi ya wanawake jijini Tanga wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya ziara yake Mkoani Tanga ambayo imechochea kasi ya maendeleo katika miradi mbalimbali.
Mwanahawa Ally Mwalimu ni mmoja kati ya wanawake waliotoa shukrani zao kwa Rais ambapo wamemuomba kuweka msisitizo katika suala zima la mikopo inayotolewa na serikali iweze kuwafikia ipasavyo.
"Tunamshukuru Mama Samia kwa kututembelea sisi wanatanga pia tunafurahi kwa yote yanayoendelea kwenye bandari yetu kikubwa ambacho tunatamani mama aongeze ni mawakala katika bandari ya Tanga kwani kupitia bandari yetu watoto wetu wanapata ajira lakini pia na mji wetu unazidi kukua kimaendeleo, "amesisitiza Evelyn Mshana Mkazi wa jiji la Tanga.
Rais Dkt. Samia amehitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani Tanga ambayo imedumu kwa siku saba katika ziara hiyo amezindua na kukagua miradi mbalimbali yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 3.1 fedha ambazo zimeelekezwa Mkoani Tanga kwajili ya maendeleo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake kama Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania. 





















Social Plugin