Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Oddo Mwisho akizungumza na wananchi wa Kata ya Gumbiro
Mwenyekiti Oddo Mwisho akipokelewa na vijana wa skauti kwa kuvishwa skafu Kata ya Wino Halmashauri ya Madaba Songea
Wanachama na wananchi waliojitokeza kumsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho
Na Regina Ndumbaro-Madaba Songea.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa, Oddo Mwisho, amewatahadharisha baadhi ya viongozi wa chama wanaojichukulia sheria mikononi kwa kuwaondoa wenzao madarakani bila kufuata taratibu.
Akizungumza katika ziara yake katika kata ya Wino na Gumbiro, Mwenyekiti huyo amewataka viongozi kufuata sheria na kanuni za chama ili kudumisha mshikamano na maendeleo ya chama hicho.
Katika ziara yake, Mwenyekiti Oddo Mwisho amesisitiza kuwa maendeleo ya chama yanategemea kuwajali wananchi na viongozi wake.
Amebainisha kuwa Ilani ya CCM inaelekeza namna ya kufanya maamuzi kwa kufuata taratibu rasmi, hivyo viongozi wanaokiuka sheria wanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za chama.
Aidha, ameagiza viongozi waliowekwa pembeni bila kufuata utaratibu warejee katika majukumu yao mara moja.
Mwenyekiti huyo pia ametumia fursa hiyo kujibu maswali ya wananchi wa Kata ya Wino na Gumbiro, waliohoji kuhusu changamoto za upatikanaji wa maji safi, umeme, na miundombinu ya barabara.
Amewahakikishia wananchi kuwa serikali na chama vinaendelea kushughulikia changamoto hizo kwa kuhakikisha miradi muhimu ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.
Katika hatua nyingine, Oddo Mwisho amewapongeza wananchi wa kata hizo kwa ushindi mkubwa walioupata katika uchaguzi wa vitongoji kupitia CCM.
Amesema ushindi huo ni ishara ya imani kubwa ya wananchi kwa chama hicho, ambacho kimejidhatiti kuendelea kuongoza dola na kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Amesisitiza kuwa CCM ni chama cha haki na wajibu, hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kusimamia maendeleo ya maeneo yao.
Mwenyekiti huyo pia amewataka wananchi kuendelea kudumisha nidhamu na kuheshimu mali za umma na rasilimali za kijiji.
Amesisitiza kuwa chama lazima kiwe na nidhamu kwa wananchi wake kwa kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mmoja.
Aidha, amewahimiza wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao ili kuimarisha demokrasia na maendeleo ya taifa.
Baadhi ya, wananchi waliohudhuria mkutano huo, akiwemo Casto Joseph Mgaya na Albert Elnaus, wamempongeza Mwenyekiti Oddo Mwisho kwa kutembelea maeneo yao na kusikiliza changamoto zao.
Pia wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo na kuimarisha ustawi wa chama na taifa kwa ujumla.
Social Plugin