Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha
Na Marco Maduhu,Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne ya utawala wake na kusema kwamba katika kipindi hicho, Rais Samia amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mkoa huo.
Amesema katika kipindi cha utawala wa Rais Samia, mkoa wa Shinyanga umepewa kiasi cha fedha cha shilingi trilioni 1, na fedha hizi zimewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Macha ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya Rais Samia kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania awamu ya sita, baada ya kifo cha Rais Hayati John Pombe Magufuli, kilichotokea Machi 17, 2021.
Amesema kuwa baada ya Rais Samia kuchukua uongozi, alionyesha kujituma kwa kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwatumikia wananchi.
Katika kipindi cha miaka minne, mkoa wa Shinyanga umeona mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo ambayo imechangia katika kuboresha maisha ya wananchi wa mkoa huo.

“Machi 19 ni siku ambayo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania awamu ya sita, mara baada ya Hayati Rais John Pombe Magufuli kufariki dunia Machi 17,2021, Mkoa wa Shinyanga tunampongeza Rais Samia kutimiza miaka minne ya utawala wake, na amefanya kazi kubwa kuwatumikia Watanzania,”amesema Macha.
“Tukizungumzia tu kwa mkoa wa Shinyanga ndani ya miaka minne ya Rais Samia, miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa ukiwamo ujenzi wa uwanja wa ndege ambao miaka mingi ulishindwa kukamilika wenye thamani ya sh.bilioni 52,”ameongeza Macha.
Amesema kwa upande wa miundombinu ya barabara, barabara nyingi zimejengwa, na sasa barabara ya kutoka Kahama kwenda Kakola ya kilomita 73 inajengwa kwa kiwango cha lami sh.bilioni 101.
Amegusia pia miradi ya maji, kwamba wananchi wengi wamefikiwa na huduma hiyo, na bado miradi mingine inaendelea kutekelezwa, na hadi ifikapo mwishoni wa mwaka 2025 wananchi wa vijijini watakuwa na maji kwa asilimia 85.
Amesema kwa upande wa umeme katika vijiji 506 vya mkoa huo tayari vyote vina umeme, na kwamba sasa hivi unapelekwa ngazi ya vitongoji, huku akimpongeza pia Rais Samia kwa kupigania matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa huduma za afya,halmashauri zote za mkoa huo zina hospitali za wilaya,pamoja na kuikamilisha hospitali ya rufaa ya mkoa huo, na sasa wananchi wanapata huduma za kibingwa hapo hapo Shinyanga.
Amesema kwa upande wa elimu, shule nyingi mpya zimejengwa za sekondari na msingi, pamoja na kuongeza vyumba vya madarasa kwa shule ambazo zilikuwa na idadi nyingi ya wanafunzi, pamoja na kuendelea kutoa fedha za elimu bila malipo.
“Mungu aendelee kumpigania afya njema Rais Samia, ili aendelee kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo,”amesema Macha.
Amesema pia wanamuombea Hayati Rais John Pombe Magufuli ampumzike kwa Amani, na kwamba katika mkoa huo wa Shinyanga wataendelea kuyaenzi mambo mema ambayo aliyafanya katika taifa hili.
Nao baadhi ya wananchi wa Shinyanga,kwa nyakati tofauti wamemombea Hayati Rais Magufuli apumzike kwa Amani, huku wakimpongeza Rais Samia kwa kuvaa viatu vyake na kusimamia utekelezwaji wa miradi ya maendeleo, ikiwamo ya kimkakati kama vile Reli ya SGR, na daraja la Magufuli.
Hayati Rais John Pombe Magufuli,alikuwa Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2021, alipofariki dunia Machi 17 mwaka huo katika Hospital ya Mzena Jijini Dar es salaam kwa maradhi ya moyo, na kisha aliyekuwa Makamu wake wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuchukua kiti hicho, na kuapishwa Machi 19 na sasa amefikisha miaka minne ya utawala wake.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin