Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIMU WA MASOMO YA HISABATI NA KIINGEREZA DODOMA WANOLEWA



Na.Francisca Mselemu - Habari - DODOMA  RS

Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mkoa wa Dodoma Mwalimu Vincent B. Kayombo leo Machi 13, 2025 amefungua mafunzo ya siku mbili kwa walimu wa masomo ya Kiingereza na Hisabati katika ukumbi wa Mikutano wa Kondoa Irangi uliopo wilayani Kondoa.

Akizungumza kwenye hotuba yake Mwl. Kayombo amesema; "Shule Bora wamekuwa wadau muhimu katika kushirikiana na Serikali kuinua kiwango na  ubora wa elimu kwa kutoa mafunzo kwa walimu.
Mwenendo wa ufaulu  wa Mkoa wa Dodoma ni mzuri kwani katika mitihani ya Taifa ya darasa la Saba mwaka 2024 Mkoa ulifaulisha kwa 87.89% kwa kushika nafasi ya 4 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara, kadhalika katika  upimaji wa Kitaifa wa darasa la Nne, mkoa ulifaulisha kwa 94.64% na ulishika nafasi ya tatu Kitaifa. 

Kwa upande wa Sekondari Mkoa umepandisha ufaulu, idadi ya wanaofanya vizuri kidato cha Pili na cha Nne kwa ufaulu wa  daraja la Kwanza hadi la Tatu imeendelea kuongezeka kutoka 30% mwaka 2023 hadi 30.7% 2024.

"Hata hivyo pamoja na Mkoa kufanya vizuri, tuliona bado tuna jambo la kufanya, tulifanya tathimini na katika tathmini hiyo tulibaini changamoto mbalimbali, moja wapo ni baadhi ya Shule kutofanya vizuri kwenye masomo ya Kiingereza na Hesabu. Ninawapongeza na kuwashukuru Shule Bora kwa kukubali kutoa mafunzo haya”

Aidha, amewaasa Washiriki wa mafunzo hayo kutumia muda wao kujifunza, kwani anaamini watakapotulia  na kufuatilia mafunzo hayo kwa umakini, yatakuwa na tija kwao, Shule walizotoka na Mkoa kwa ujumla.

“Mnahitaji kuwa na ‘Proper attention’ mahali hapa pawepo na utulivu wa kutosha, hii sio semina ya kawaida. Mmekuja hapa kujifunza, kupewa uzoefu. Kinachotakiwa mseme kweli kwa dhati kabisa. Ukipewa nafasi ya kusema funguka. Hapa tumekuja kama wataalamu wa elimu, tuelekezane, ukiondoka na uliyokuja nayo, hujatupatia yale mazuri hujatusaidia sisi wala Mkoa.

Katika hatua nyingine Kayombo amewaagiza Maafisa Elimu (W) kuhakikisha  wanakwenda  kuwatumia walimu walioshiriki mafunzo hayo kuwapatia walimu wengine maarifa watakayoyapata. Na kwamba ana imani kubwa na Maafisa Elimu hao kwamba  watafanya bidii, ambayo italeta matokeo chanya katika mitihani ya mwaka huu.

Mradi wa Shule Bora ulianza mwaka 2021 na utamalizika 2027, ukitekelezwa katika mikoa tisa ambayo  Dodoma, Mara, Pwani, Katavi,Tanga, Simiyu, Rukwa, Kigoma na Singida, chini ya ufadhili wa Serikali ya Uingereza kupitia ‘UK – Aid’.

Mafunzo yatafanyika katika mikoa yote ya mradi, Dodoma ni mkoa wa Nne kupatiwa mafunzo hayo ukitanguliwa na Tanga, Pwani na Kigoma.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com