Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUWASA RUVUMA YAPANDA MITI 1,000 KUHIFADHI CHANZO CHA MAJI LITENGA


Wananchi waliojitokeza katika wiki ya Maji kupanda miti kijiji cha Lipokela mkoani Ruvuma
Mwananchi akipanda mti katika kijiji cha Lipokela mkoani Ruvuma
Sehemu ya Miti iliyopandwa katika kijiji cha Lipokela mkoani Ruvuma katika kilele cha wiki ya maji
Mkuu wa Ofisi ya Bonde la Ruvuma Ndogo Pwani ya Kusini, Deusdedith Gonelamende, akionesha miti inayopandwa katika kijiji cha Lipokela
Na Regina Ndumbaro Ruvuma. 

 Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Ruvuma imeanza kampeni ya kupanda miti 1,000 katika chanzo cha maji cha Litenga, kilichopo kata ya Lipokela. 

Hatua hii imelenga kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha huduma endelevu kwa wananchi. 

Mkuu wa Ofisi ya Bonde la Ruvuma Ndogo Pwani ya Kusini, Deusdedith Gonelamende, amesema upandaji huu wa miti ni utekelezaji wa Sheria Namba 11 ya mwaka 2009, inayotaka maeneo ya vyanzo vya maji yahifadhiwe kwa umbali wa mita 60 au zaidi, kulingana na mazingira.

Mhandisi Sheila Michael Kimweri kutoka ofisi ya meneja RUWASA wilaya ya Songea ameweka wazi kuwa mradi wa maji wa Litenga, wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 700, umenufaisha wakazi 2,350. Tayari miundombinu yake imekamilika kwa asilimia 96, ikiwa ni pamoja na tenki la maji lenye ujazo wa lita 100,000, banio la maji, jengo la mashine za kusukuma maji na mtandao wa mabomba wa kilomita 20. 

Pia, kuna vituo 18 vya kuchotea maji ambavyo vimeanza kutumiwa na wananchi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lipokela, JohnBosco Francis Nchimbi, ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mradi huu. 

Ameeleza kuwa hapo awali, wakazi wa eneo hilo walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa kwao. Amewataka wananchi kushirikiana katika kutunza vyanzo vya maji na kuepuka shughuli za kilimo kandokando ya mito ili kuhakikisha mradi huo unadumu kwa muda mrefu.

Wananchi wa kijiji cha Lipokela wameeleza furaha yao kwa kupata huduma ya maji safi na salama, wakisisitiza kuwa wako tayari kushirikiana na RUWASA katika kuhifadhi mazingira. 

Wamesema wanatambua umuhimu wa kuhifadhi uoto wa asili kwa ajili ya uhakika wa maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kampeni hii ya upandaji miti ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji ambayo ilianza tarehe 16 Machi na itahitimishwa tarehe 22 Machi 2025. 

Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa Uhakika wa Maji", ikisisitiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu ya jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com