
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Bodi mpya ya Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imefanya ziara ya kutembelea utekelezaji mradi wa mtambo wa kuchakata tope taka unaolenga kuboresha huduma za usafi wa mazingira kwa wananchi wa Shinyanga huku ikipongeza hatua zilizofikiwa katika upanuzi wa mtambo huo wa kisasa ambapo kwa sasa umefikia asilimia 98 ya utekelezaji.
Ziara hiyo imefanyika leo Februari 13, 2025 na bodi ya (SHUWASA) kufanya ukaguzi wa mradi huo uliopo kata ya Kizumbi ndani ya manispaa
ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo ,Mwenyekiti wa bodi hiyo Bi Mwamvua Jilumbi ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) kwa kufanya upanuzi wa eneo la mradi huo na kuepuka kusimama kwa shughuli za uchakataji wa tope taka kulingana na ufinyu wa eneo uliokuwepo hapo awali huku akimpongeza mkandarasi kwa hatua nzuri ya utekelezaji wa upanuzi wa mradi huo ulipofikia.
“Kama bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Shinyanga SHUWASA tumeridhishwa na utekelezaji huu wa mradi unaofanya na
SHUWASA kwa kweli thamani ya fedha inayotumika tunaiona na tuipongeze menejimenti
ya SHUWASA kwa kuamua kuongeza eneo hili la mradi wa uchakataji wa tope taka ni
matumaini yetu sasa mradi huu utaendelea kufanya kazi vizuri, lakini pindi
mradi huu utakapo kamilika nitoe rai ukusanyaji wa mapato kwa uangalifu mkubwa
kwa sababu mapato yakipatikana itawezesha mamlaka kufanya miradi mingine ya
kimaendeleo na manufaa makubwa”, amesema Bi Mwamvua.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi huo Msimamizi wa uborehaji wa
mradi kutoka (SHUWASA) Mhandisi Wilfred Julias amesema utekelezaji wa mradi umefikia
asilimia 98 na kubainisha kuwa lengo la mradi huo ni kuongeza uwezo wa mtambo
ili kukidhi mahitaji.
“Mtambo ulkuwa na uwezo wa kuchakata mita za ujazo 40 za
tope taka kwa siku lakini baada ya upanuzi kukamilika utafikia hadi mita za
ujazo 100 kwa siku”, amesema Mhandisi Wilfred.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Shinyanga
SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola amesema upanuzi wa mtambo huo utakwenda kukuza
pato la ukusanyaji lakini pia kukidhi mahitaji ya ukusanyaji wa tope taka
kutoka majumbani lengo likiwa ni kuendelea kuweka manispaa ya Shinyanga katika
hali ya usafi na kuendeleza heshima ya kuwa manispaa inayoongoza kwa usafi
nchini.



Social Plugin