Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDUMBARO AMPOKEA KADA WA CHADEMA ALIYETIMKIA CCM

Waziri wa Sheria na Katiba Dkt. Damas Ndumbaro akisalimiana na kada wa CHADEMA aliyehamia Chama cha Mapinduzi (CCM)
Waziri wa Sheria na Katiba Dkt. Damas Ndumbaro na Mbunge wa Songea Mjini akionesha kadi ya mwanachama wa CHADEMA aliyehamia Chama cha Mapinduzi (CCM)
Osmund Mapunda akivalishwa Shati la Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati akirejesha kadi yake ya awali ya uanachama kupitia CHADEMA

Na Regina Ndumbaro -  Ruvuma

Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Songea Mjini, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, amempokea rasmi aliyekuwa kiongozi wa CHADEMA katika Kata ya Lilambo, Osmund Mapunda, na kumkabidhi kadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hafla hiyo imefanyika mbele ya wananchi wa kata hiyo wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa stendi ya maegesho ya maroli katika eneo hilo.

Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali pamoja na wanachama wa CCM.

Akizungumza mara baada ya kupokea kadi ya CCM, Mapunda amesema kuwa amehamia chama hicho kutokana na kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya CCM katika Jimbo la Songea Mjini.

Ameeleza kuwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa ni yenye tija kwa wananchi na inatoa suluhisho kwa changamoto zao.

Mapunda amesema uamuzi wake si wa shinikizo bali umetokana na tathmini ya kina kuhusu mwelekeo wa maendeleo ya Songea Mjini. Amesema CCM imeonesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa vitendo.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Ndumbaro amempongeza Mapunda kwa hatua yake na kusema kuwa CCM ni chama kinachowakaribisha wote wenye nia njema ya kuleta maendeleo.

Amesema kuwa chama hicho kitaendelea kushirikiana na wanachama wapya na wa zamani kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote.


Katika hotuba yake, Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, hospitali, na miundombinu ya elimu na kwamba miradi hii inalenga kuboresha maisha ya wananchi wa Songea Mjini.

Wananchi wa Kata ya Lilambo wameonyesha kufurahishwa na uamuzi wa Mapunda, wakisema kuwa ni ishara ya imani kwa serikali ya CCM.


Wamesema kuwa maendeleo yanayoonekana katika eneo hilo ni matokeo ya uongozi imara wa chama hicho.

Hafla hiyo imehitimishwa kwa sherehe fupi ambapo viongozi wa CCM wamemkabidhi rasmi Mapunda kadi ya chama, huku wakimhakikishia ushirikiano wa dhati katika shughuli za kisiasa na maendeleo ya Songea Mjini.

Kwa mujibu wa viongozi wa CCM, chama hicho kitaendelea kupokea wanachama wapya kutoka vyama mbalimbali na kuwapa nafasi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com