Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri akisalimiana na Chifu Emanuel Zulu Gama wakati wa Ufunguzi wa maadhimisho ya mashujaa wa Vita ya Majimaji Mkoani Ruvuma

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Peres Magiri akitoa hotuba ya taarifa ya mashujaa hao waliopambana dhidi ya wakoloni
Picha ya pamoja ya Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu Wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri ambae ni mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Kanali Ahmed Abbas Ahmed
Na Regina Ndumbaro-Ruvuma.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mheshimiwa Peres Magiri, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameongoza uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya kumi na tano ya mashujaa.
Maadhimisho haya yamezinduliwa katika viwanja vya Makumbusho Mkoani Ruvuma kwa mara ya kwanza maadhimisho haya yalizinduliwa rasmi mnamo mwaka 2010 ili kuwaenzi mashujaa waliopambana dhidi ya wakoloni wa Kijerumani mnamo mwaka 1906.
Katika mapambano hayo, mashujaa 67 walinyongwa na kuzikwa katika kaburi moja, huku Chifu Nduna Songea Mbano akizikwa katika kaburi lake peke yake.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Magiri ameeleza kuwa ndugu wa mashujaa hao wanaiomba serikali ifanye juhudi za kurejesha baadhi ya viungo vya wapendwa wao ambavyo vilichukuliwa na wakoloni wa Kijerumani.
Amesema kwamba hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha historia ya mashujaa hao inahifadhiwa na kuthaminiwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Mwalimu Siwetu, Mkuu wa Shule ya Msingi Bombambili na Mwenyekiti wa Shule za Msingi mkoa wa Ruvuma, aliweka wazi kuwa maadhimisho haya yana lengo la kuwaenzi mashujaa waliopigania uhuru wa nchi.
Amesema kuwa ni muhimu kwa kizazi cha sasa kufahamu historia ya mababu zao na namna walivyojitolea kupinga utawala wa kikoloni wa Kijerumani.
Mwalimu Siwetu ameeleza kwa kina kuhusu kaburi la mashujaa 67 waliozikwa pamoja na kaburi la pekee la Chifu Nduna Songea Mbano.
Amesema kuwa mashujaa hao walionesha uzalendo wa hali ya juu kwa kujitoa mhanga ili kuikomboa nchi yao kutoka mikononi mwa wakoloni.
Aidha, amefafanua kuwa maadhimisho haya pia yana malengo ya kuwaelimisha wanafunzi kuhusu urithi wa utamaduni wa Kingoni, historia ya machifu mbalimbali waliopambana na wakoloni katika maeneo tofauti ya Tanzania, na umuhimu wa kupigania haki na uhuru wa nchi kwa moyo wa uzalendo.
Mwanafunzi Tariki Juma Abdalah wa Shule ya Sekondari Bombambili amezungumzia maadhimisho haya kama fursa muhimu ya kujifunza historia ya Waafrika na jinsi wakoloni wa Kijerumani walivyofika barani Afrika na kuwatendea unyama mababu zao.
Amesema kuwa kupitia historia hii, vijana wanajifunza thamani ya mshikamano na uzalendo.
Akitoa mfano wa Chifu Nduna Songea Mbano, Tariki ameeleza kuwa chifu huyo alikubali kujitoa kwa wakoloni ili kuwaokoa wananchi wake.
Amewahimiza vijana wa kizazi cha sasa kuwa wavumilivu, wenye msimamo thabiti, na kuenzi utamaduni wa Taifa lao kwa kuendelea kuipenda na kuitetea Tanzania.
Maadhimisho haya yameleta mwamko mkubwa wa kihistoria kwa jamii, hasa kwa vijana, ambao sasa wanapata uelewa wa kina kuhusu historia ya mashujaa wa Tanzania.
Serikali na wadau mbalimbali wanaendelea kushirikiana kuhakikisha historia hii inaendelezwa kwa vizazi vijavyo ili kuhakikisha kuwa mchango wa mashujaa wetu haupotei.
Social Plugin