Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA MKOA WA SHINYANGA AZINDUA KAMPENI HARAKISHI YA KUIBUA WAGONJWA WENYE VIMELEA VYA UGONJWA WA KIFUA KIKUU

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, akizungumza wakati akizindua Kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu katika mkoa wa Shinyanga

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, amezindua Kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu katika mkoa wa Shinyanga, huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupima ugonjwa huu hatari na kuanza matibabu mara moja, ambayo yatatolewa bure.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo leo Februari 8, 2025, Mhe. Macha amesema kuwa lengo kuu la kampeni hii ni kuwasaka wananchi 1,349 waliobaki na ambao bado hawajafikiwa na huduma za matibabu, kati ya watu 2,903 wanaokadiriwa kuwa na vimelea vya kifua kikuu katika mkoa huu.

 "Ugonjwa huu ni hatari na unaambukizwa kwa njia ya hewa, hivyo ni muhimu hatua zichukuliwe mapema," amesisitiza.

Mhe. Macha ameeleza kuwa kila mtu mwenye kifua kikuu ana uwezo wa kuambukiza hadi watu 20 kwa mwaka mmoja, hivyo tatizo linaweza kuwa kubwa kama hatua za haraka hazitachukuliwa.

 Ameongeza kuwa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia kampeni hii, inalenga kuokoa afya za wananchi na kupunguza maambukizi.

Amesema kuwa wakati wa matibabu, wananchi wanapaswa kumaliza dozi zote za dawa za kifua kikuu ili kuepuka kuundwa kwa usugu wa ugonjwa huo, hali ambayo inasababisha ugonjwa kuwa ngumu kutibika.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Luzila John, ametoa takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2023, zikionesha kuwa watu milioni 10.8 waligundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu, na milioni 2.5 walifariki dunia. 

Amebainisha kuwa kifua kikuu kinawaathiri zaidi watu katika nchi za Asia na Afrika, na amesema dalili kuu za ugonjwa huu ni kukohoa muda mrefu, homa, kupungua uzito, kutokwa jasho usiku, na maambukizi kwa njia ya hewa.

Dkt. Luzila ameongeza kuwa aina mbalimbali za kifua kikuu zipo, ikiwa ni pamoja na TB ya Moyo, Mifupa ya Mgongo, Ubongo, na TB ya Mapafu, na alieleza kuwa katika uchunguzi uliofanywa Januari 2025, watu 6 kati ya 84 waligundulika kuwa na vimelea vya kifua kikuu, na Februari, watu 3 kati ya 28 waligundulika kuwa na ugonjwa huu na walianza kupata matibabu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Ndungile, ameeleza kuwa kampeni hii harakishi inalenga kuwasaka wagonjwa wa kifua kikuu ambao hawajafikiwa na huduma, na lengo ni kuwafikia watu 1,349 ili kuwapatia matibabu na kuhakikisha hawaambukizi tena.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, amesema kampeni hii ni endelevu na inaratibiwa na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, na wadau wa kupambana na kifua kikuu. Alisisitiza kuwa huduma zote zinazotolewa kupitia kampeni hii ni bure kwa wananchi.

Wananchi wa Shinyanga, kama Magera Seni, ambaye amejitokeza kupima vimelea vya kifua kikuu, wameshukuru serikali kwa kuanzisha kampeni hii, wakiwa na matumaini kuwa itaokoa maisha ya wengi kwa kutoa matibabu bure na kuzuia maambukizi zaidi.

Kampeni hiyo inatoa fursa muhimu kwa wananchi wa Shinyanga kupata huduma ya bure ya kupima kifua kikuu, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kujitokeza kwa wingi na kuchukua hatua za afya kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu hatari.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi kuibua wagonjwa wa kifua kikuu. 
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salumu Hamduni akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu.
Uzinduzi wa kampeni ya harakishi ya kuibua wagonjwa wa kifua kikuu ukiendelea.

Picha ya pamoja ikipigwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com