Mafundi wakiendelea na ujenzi wa kioski cha kuchotea maji katika kijiji cha Kimbanga Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma.

Na Regina Ndumbaro, Nyasa.
Wananchi wa Kijiji cha Kimbanga, Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wamepata matumaini mapya baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa Shilingi milioni 60 kwa ajili ya uchimbaji wa kisima cha maji safi na salama.
Hatua hii imelenga kumaliza changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji, hali ambayo imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.
Kwa muda mrefu, wakazi wa Kimbanga walilazimika kutembea kati ya kilometa 1 hadi 2 kila siku kwenda vijiji jirani kutafuta maji.
Changamoto hii imeathiri shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo cha mazao ya chakula na biashara kama kahawa.
Kutokana na hali hiyo, serikali imechukua hatua madhubuti kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji safi na salama karibu na makazi yao.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Nyasa, Athuman Chola, amesema kuwa serikali imetoa Shilingi milioni 300 kwa ajili ya uchimbaji wa visima vitano wilayani humo.
Kijiji cha Kimbanga ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huu, ambapo ujenzi wa kisima umekamilika na kwa sasa mafundi wanaendelea na ujenzi wa kioski cha kuchotea maji, ambacho kimefikia zaidi ya asilimia 40 ya utekelezaji.
Kwa mujibu wa Chola, kazi zinazoendelea ni pamoja na usambazaji wa mabomba ya maji kwenda kwenye makazi ya wananchi, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, ufungaji wa mashine ya kusukuma maji kutoka kwenye kisima hadi kwenye tenki, pamoja na uwekaji wa umeme jua ili kuhakikisha mradi unafanya kazi kwa ufanisi.
Hata hivyo, katika vijiji vinne kati ya vitano vilivyopangwa kunufaika na mradi huu, uchimbaji wa visima haujafanikiwa kupata maji chini ya ardhi.
Chola amesema kuwa RUWASA itatumia mbinu mbadala kama kuboresha chemchem zilizopo na kujenga miradi ya mserereko kwa kutumia maji yanayotoka milimani ili kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama.
Katika Kijiji cha Malamala, usanifu wa mradi unafanywa upya baada ya kushindikana kupata chanzo cha maji cha uhakika.
RUWASA inashirikiana na Mamlaka ya Bonde la Ziwa Nyasa ili kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanapata maji kwa njia mbadala.
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji vijijini ili kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Baadhi ya wakazi wa Kimbanga wameelezea furaha yao kwa hatua hii ya serikali Adelius Mwingira amesema kuwa mradi wa kisima utawaondolea adha ya kutumia maji ya visima vya asili ambavyo si salama, pamoja na mateso ya kubeba ndoo za maji kichwani kila siku.
Kwa upande wake, Bonus Kapinga amesema kuwa mradi huu ni ukombozi mkubwa kwao, kwani kijiji hicho hakijawahi kupata maji ya bomba tangu kilipoanzishwa zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Aidha, Kapinga ameongeza kuwa ukosefu wa maji umeathiri maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi wa shule ya msingi, kwani muda wao wa masomo hupotea kwa kutafuta maji badala ya kusoma.
Naye William Komba ameishukuru serikali kwa kuleta mradi huu wa kisima cha maji, lakini ameomba RUWASA iharakishe kukamilisha mradi huo na kuhakikisha maji yanafika moja kwa moja kwenye makazi ya wananchi ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu hadi kwenye vituo vya kuchotea maji.
Social Plugin