Na Mwandishi wetu,Mtwara
Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kuweka kambi Mkoani Mtwara kuendesha mafunzo na utoaji wa elimu ya Uraia na Utawala Bora kwa viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata, na vijiji, sambamba na kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea kutoa huduma kwa wananchi katika halmashauri zote za mkoa huo.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kisheria kwa Umma kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Abdurahmani Mshamu, alibainisha mada zinazotolewa katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na demokrasia na utawala bora, haki na wajibu wa jamii, madaraka kwa umma, ulinzi na usalama, akisema kuwa lengo kuu ni kuboresha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Aidha, akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, alisema kuwa changamoto nyingi zinazoikumba jamii katika utekelezaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na uelewa mdogo wa misingi ya haki, mila na desturi kandamizi, pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia, amewataka wanufaika wa mafunzo hayo kwenda kuibadilisha jamii kwa kuzingatia misingi ya haki.
"Mafunzo haya yatafungua ufahamu wetu wa namna bora ya kushauri na kuongoza watu wetu, ofisi zetu zinatakiwa kuwa msaada na kimbilio kwa wananchi. Sisi viongozi, tujiulize tunafanyaje kazi na viongozi wenzetu bila kuingiliana madaraka, tunapaswa tushirikiane," alisema Kanali Sawala.
Kwa upande wa baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo, wamesema mafunzo haya yamefika wakati muafaka na kuahidi kwenda kuiongoza jamii katika misingi ya haki na utawala bora.
Social Plugin