Baadhi ya wanufaika wa mfuko wa TASAF Ruvuma
Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile
Baadhi ya washiriki wa kikao cha ngazi ya mkoa na wilaya ukumbi wa Heritage Cottage Songea mjini
Na Regina Ndumbaro Ruvuma.
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mheshimiwa Kapenjama Ndile, amesema Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Kwa mwaka 2024 pekee, Mkoa wa Ruvuma umepokea zaidi ya shilingi bilioni 12 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini.
Mheshimiwa Ndile ametoa kauli hiyo wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, wakati wa kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa mpango wa TASAF kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2024.
Kikao hicho kimehusisha wataalam kutoka ngazi ya mkoa, wilaya, na halmashauri zote za Ruvuma na kimefanyika katika ukumbi wa Heritage Cottage mjini Songea.
Katika hotuba yake, ameeleza kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuwawezesha wanufaika kuongeza kipato, kupata fursa za kiuchumi, na kuhudumia mahitaji yao muhimu.
Pia, mpango unalenga kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii, kuwekeza katika elimu ya watoto wao, na kupata maarifa ya kujikwamua kiuchumi kwa maendeleo endelevu ya jamii.
Mheshimiwa Ndile amewataka wataalam wote wanaohusika na utekelezaji wa TASAF kuhakikisha wanasimamia fedha zinazotolewa kwa uwajibikaji mkubwa.
Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia miongozo na maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha mpango huu unaleta matokeo chanya kwa wananchi maskini wa Ruvuma.
Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF Mkoa wa Ruvuma, Bi. Xsaveria Mlimira, ameeleza kuwa jumla ya kaya 47,721 zinaendelea kunufaika na mpango huo katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024.
Amebainisha kuwa kaya 18,912 tayari zimehitimu kutoka mpango huo, na kwa sasa utekelezaji wa awamu ya pili unaendelea katika vijiji na mitaa 685 kutoka wilaya zote za mkoa wa Ruvuma.
Bi. Mlimira ameongeza kuwa katika kipindi hicho cha mwaka 2024, Mkoa wa Ruvuma umepokea jumla ya shilingi bilioni 12.8 kwa ajili ya uhawilishaji wa fedha kwa walengwa pamoja na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mpango huo.
Fedha hizo zimeelekezwa moja kwa moja kwa wanufaika ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Baadhi ya wanufaika wa mpango huo wameelezea manufaa waliyoyapata kupitia TASAF. Bi. Regina Komba, mmoja wa wanufaika, amesema mpango huo umemwezesha kuwasomesha watoto wake, jambo ambalo asingeliweza kufanya kutokana na hali ngumu ya maisha aliyokuwa nayo kabla ya kunufaika na TASAF.
Mnufaika mwingine, Bi. Suzan Komba, ameeleza kuwa kupitia mpango wa TASAF, ameweza kuanzisha miradi mbalimbali ya ufugaji wa kuku na nyuki.
Miradi hiyo imemsaidia kuboresha maisha yake na sasa anaweza kuendesha shughuli zake za kila siku kwa uhuru na bila changamoto kubwa za kiuchumi.
Social Plugin