Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUWASA YATAMBULISHA MRADI WA MAJI MBANGA NA LUMEME WENYE THAMANI YA MILIONI 962

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa Masoud Samila ()kulia akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri Mkataba wa ujenzi wa mradi huo maji vijiji viwili Mbanga na Lumeme
Mkuu wa Wilaya wa Nyasa Peres Magiri akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mbanga kabla ya kutambulisha mradi mkubwa wa maji
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Peres Magiri hayupo kwenye picha wakati wa hafla fupi ya kutambulisha mradi wa maji

Na Regina Ndumbaro - Nyasa.

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma umetambulisha mradi wa maji wenye thamani ya Shilingi milioni 962.7 unaotarajiwa kutekelezwa katika vijiji vya Mbanga na Lumeme. 

Mradi huu unalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji hivyo, na unatarajiwa kuhudumia watu wapatao 4,990.

Akizungumza katika hafla ya kutambulisha mradi huo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya serikali ya kijiji cha Mbanga, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, amewataka wakandarasi kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa viwango vya juu na kukamilika kwa wakati.

 Magiri amewataka wananchi kushirikiana na mkandarasi kwa kulinda vifaa vya ujenzi na kutunza vyanzo vya maji ili mradi uwe endelevu.

“Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kutatua kero ya maji. Mkandarasi hakikisha unajenga mradi kwa ubora ili maji yatoke. Wananchi pia tunapaswa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huu kwa kuwa ni wa kwetu," amesema Magiri.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa, Mhandisi Masoud Samila, amesema mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya CONSEL Construction and Engineering Services Co. Ltd kutoka Mwanza. Kazi za mradi ni pamoja na ujenzi wa mtego wa maji, tanki la kuhifadhi lita 150,000, ulazaji wa mabomba kilomita 32, ujenzi wa bomba kuu la kilomita moja, na ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji.

Mhandisi Samila ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita, kufikia tarehe 6 Aprili mwaka huu. Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na mkandarasi ili kazi ikamilike kwa wakati na kuondoa adha ya maji inayowakabili. Amesema mradi huo pia utapunguza magonjwa ya mlipuko kwa kuboresha huduma ya maji safi na salama.


Wananchi wa vijiji vya Mbanga na Lumeme wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya. Mbunge huyo amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa manufaa ya jamii.

“Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeendelea kushughulikia kero za wananchi, na huu ni mfano wa jitihada hizo. Naomba muendelee kuwa na imani na Serikali, kwani tunaendelea kuboresha maisha na kukuza uchumi wa wananchi,” amesema Manyanya.

Mradi huu unatazamiwa kuwa mkombozi kwa vijiji vya Mbanga na Lumeme, ambapo wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi kwa muda mrefu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com