CWT BAGAMOYO YATUNUKU MAJIKO YA GESI KWA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI CHALINZE

Baadhi ya walimu wakipokea majiko ya gesi kutoka kwa uongozi wa CWT Wilaya ya Bagamoyo


NA. ELISANTE KINDULU,CHALINZE

CHAMA cha walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Bagamoyo kimesambaza majiko 25 ya gesi katika shule mbalimbali za msingi na sekondari katika halmashauri ya Chalinze.

Akigawa majiko hayo kwa wawakilishi wa CWT mahala pa kazi leo katika kituo cha walimu Chalinze , Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Bagamoyo Mwalimu Hamisi Kimeza, alieleza kuwa hiyo ni sehemu tu ya misaada ya chama dhidi ya shule za msingi na sekondari wilayani Bagamoyo. 

Mwenyekiti huyo alieleza kwamba chama kimekuwa na utamaduni wa muda mrefu kusaidia shule kwa vifaa mbalimbali ila katika hili la ugawaji wa majiko wapo sambamba na  jitihada za Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan za kupambana na uharibifu wa mazingira.

Naye katibu wa Chama hicho Wilaya ya Bagamoyo Mwalimu Joyce Maisa waliwaambia wawakilishi hao kuwa kila shule itafikiwa na jiko ili kuwafanya walimu kupata chakula kwa pamoja huku wakijadili masuala mbalimbali yanayowahusu.

"Leo tutagawa majiko 25, japo tulishaanza hili zoezi kwa siku za nyuma kwa baadhi ya shule kupata na mgao huu. Tunatarajia kuzimaliza shule zote katika kipindi kifupi kijacho ili tuangalie kipaumbele kingine kwa wanachama wetu", alisema katibu Maisa.

Shule zilizonufaika katika awamu hii  ni kutoka Kata za Kiwangwa , Lugoba , mandera na Vigwaza







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post