AMREF TANZANIA WAKABIDHI SIMU JANJA KWA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII SHINYANGA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

 

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

SHIRIKA la Amref Health Africa -Tanzania kupitia mradi wa Thamini Uzazi Salama (Strengthening Midwifery project), limekabidhi simu janja 56 kwa hudumu wa afya ngazi ya jamii mkoani Shinyanga, katika mapambano ya kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga.
Makabidhano hayo yamefanyika leo Septemba 23,2024 katika Ofisi za Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Yudas Ndungile, yakihudhuriwa pia na wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wamekabidhiwa simu hizo.

Meneja programu kitengo cha Afya ya Uzazi, Mama, watoto wachanga na vijana kutoka Amref Dkt. Serafina Mkuwa, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi simu hizo, amesema wahudumu hao wa afya ngazi ya jamii 56 mkoani Shinyanga, wamepewa mafunzo ya jinsi ya kutumia program ya LEAP, ambayo inawawezesha kupata moduli za mafunzo ya afua za mama na mtoto.

“Leo tupo mkoani Shinyanga kukabidhi simu janja kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 56, wanaume 33 na wanawake 23, simu hizi zitatumika si tu kuboresha maarifa na ujuzi, bali pia kuimarisha ufanisi wa jumla wa mifumo ya utoaji wa huduma za afya za jamii, kama vile uboreshaji wa rufaa, kurahisisha mawasiliano,kuimarisha ukusanyaji takwimu zinazohusiana na huduma za afya za mama na mtoto na uandikishaji wa bima ya afya CHF iliyoboreshwa,”amesema Serafina.

Amesema makabidhiano ya simu hizo janja kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa thamini uzazi salama, ambapo Amref wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Wizara ya Afya na TAMISEMI, katika eneo la kuboresha na kuimarisha afya ya mama na mtoto.
“Mradi huu unafadhiliwa na GAC na kusimamiwa na UNFPA na unalenga kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga, kwa kuongeza upatikanaji wa wakunga wenye ujuzi nchini Tanzania, na unalenga taasisi za mafunzo ya afya, vituo vya wahuduma za afya na wafanyakazi wa afya wakiwamo wauguzi, wakunga, wanajamii na wadau wa serikali,”amesema Serafina.

Ameongeza "Mradi huu unatekeleza mikakati ya jamii inayolenga kuwa elimisha wanajamii kuhusu upatikanaji,ufikiwaji na matumizi ya huduma za mama na mtoto, miongoni mwa mikakati hii ni pamoja na kufanya kazi na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kwa kuwajengea uwezo ili waweze kutoa huduma bora na stahiki za mama na mtoto".
Aidha, amesema wahudumu hao wa afya ngazi ya jamii na viongozi wao, awali walishapewa mafunzo hayo na bado wanaendelea na masomo kupitia program ya LEAP na mafunzo hayo yalishafanyika mwezi wa nane, na yanajumuisha moduli 13 za afya za mama na mtoto, na kwamba hadi sasa wameshafikisha moduli ya tano, na wamewapatia simu hizo janja ambazo zinawasaidia katika masomo yao na kuisaidia jamii.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile, amelipongeza Shirika hilo la Amref kwa kusaidiana na serikali katika mapambano ya kupunguza vifo vya mama na mtoto, na kuwawezesha wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali kupitia simu janja.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Dk. Nuru Yunge akizungumza kwa niaba ya waganga wakuu wa wilaya mkoani humo, amesema, mradi huo wa Amref utasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto, na kwamba kupitia wahudumu hao wa afya ngazi ya jamii, akina mama wajawazito watahudhuria klinik kwa wingi pamoja na kujifungulia kwenye huduma za afya sehemu ambayo ni salama kutokana na kupatiwa elimu.

Mmoja wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii Getruda Emmanuel, amesema kupitia simu hizo wataendelea kujifunza mafunzo yao, na watasaidia kutoa elimu kwa jamii juu ya uzazi salama na hatimaye kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Meneja programu kitengo cha Afya ya Uzazi, Mama, watoto wachanga na vijana kutoka Amref Dr. Serafina Mkuwa akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi simu Janja 56 kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii mkoani Shinyanga.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi simu janja 56 kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii mkoani humo.
Mganga wa hospitali ya wilaya ya Shinyanga Dk. Nuru Yunge akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi simu janja 56 kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii
Mhudumu wa afya ngazi ya jamii Getruda Emmanuel akitoa shukrani kwa Amref.
Meneja programu kitengo cha Afya ya Uzazi, Mama, watoto wachanga na vijana kutoka Amref Dr. Serafina Mkuwa, (kulia) akikabidhi simu janja 56 za wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile (kushoto)akikabidhi simu janja kwa Mganga Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Dk.Nuru Yunge akiwakilisha pia Waganga wakuu wa wilaya mkoani humo.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Dk.Nuru Yunge (kushoto) akikabidhi simu janja kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Wahudumu wa afya ngazi ya jamii wakionyesha simu janja.
Meneja programu kitengo cha Afya ya Uzazi, Mama, watoto wachanga na vijana kutoka Amref Dr. Serafina Mkuwa,(kulia) akiwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile wakisaini makabidhiano ya simu janja 56 za wahudumu wa afya ngazi ya jamii mkoani humo.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Dk.Nuru Yunge akisaini makabidhiano ya simu janja za wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Meneja programu kitengo cha Afya ya Uzazi, Mama, watoto wachanga na vijana kutoka Amref Dr. Serafina Mkuwa (kulia)akikabidhiana hati za makabidhiano za simu janja 56 za wahudumu wa afya ngazi ya jamii na Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya simu janja 56 za wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutoka Amref.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Picha ya pamoja ikipigwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post