TEMBO WAENDELEA KUHATARISHA MAISHA YA WAKAZI WA UMBA - LUSHOTO


Mbunge wa Jimbo la Mlalo Rashid Shangazi 

Na Hadija Bagasha - Lushoto

 Changamoto ya uvamizi wa tembo katika makazi ya watu na mashamba imeendelea kuhatarisha maisha ya wakazi wa tarafa ya Umba Wilayani Lushoto Mkoani Tanga. 

Changamoto hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Mlalo Rashid Shangazi wakati akizungumza mbele ya Makamu wa pili wa Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah akiwa katika mkutano wake na wanachama wa chama cha mapinduzi ccm Wilayani Lushoto. 

Mbunge huyo amesema kwamba wanyama hao wameendelea kuhatarisha maisha ya watu lakini pia wamekuwa wakiathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo hayo. 

"Pamoja na jitihada kubwa ambazo serikali imeendelea kuzifanya za kuwadhibiti wanyama hawa lakoni bado wanyama hawa wameendelea kuwa tishio kwa maisha ya watu na shughuli za kiuchumi hivyo kama nchi tunaomba kupitia nafasi yako ya Mjumbe wa kamati kuu tuje na mbinu mbadala ambazo zinaweza zikawafanya wakazi wa tarafa ya umba pamoja na maeneo mengine ya nchi yetu kuweza kufanya shughuli zao kwa utulivu, amesisitiza Mbunge Shangazi.

Akizungumza katika kikao hicho Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah amewahakikishia wana Lushoto kwamba changamoto zilizowasilishwa mbele yake kuwa yeye kama mlezi amezichukua kwa kushirikiana na viongozi wengine kuzifikisha kwenye mamlaka husika ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi. 

"Nataka niwape imani maana ukipata imani unajenga imani kubwa kiongozi wetu Daktari Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya mengi makubwa kwa wilaya hii ni wilaya ambayo imefaidika kati ya hayo makubwa ambayo nimeyazungumza niwahakikishie salamu hizi zitafika kwa mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa chama chetu na niwaahidi kwa utaratibu ambao utafanywa atazishugulikia kama utaratibu wake,"alisema Makamu huyo

"Mwaka jana tulipokuja tulikuta changamoto tofauti nshukuru Mwenyezi Mungu baadhi ya changamoto zimeshughulikiwa mambo yanaenda vizuri msiwe na wasiwasi tujenge imani kwa Rais wetu,  tujenge imani kwa viongozi wetu pamoja na waheshimiwa wabunge wanaofanya kazi nzuri ya kutusemea na kuomba fedha ambazo tayari zimekwishawekwa kwenye bajeti kwenye badhi ya maeneo, "alisema. 

Mbunge wa jimbo la Lushoto Shaban Shekilindi ametumia mkutano huo kumshukuru Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwafikishia miradi mingi ya maendeleo wilayani humo ikiwemo ya elimu,  afya,  barabara na umeme. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post