CHADEMA KANDA YA SERENGETI YATAKA JESHI LA POLISI KUHAKIKISHA USALAMA WA RAIA NA KUHESHIMU HAKI ZA BINADAMU


Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, akitoa  taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Agosti 29,2024.

Na Mapuli Kitina Misalaba

 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Serengeti kimetoa wito kwa vyombo vya usalama, hususan Jeshi la Polisi, kuhakikisha usalama wa raia na kuheshimu haki za binadamu katika miji ya Lamadi, Busega, Maswa, na jimbo la Itilima mkoani Simiyu.

Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameeleza kuwa matukio ya hivi karibuni yameibua wasiwasi miongoni mwa wananchi, hususan baada ya tukio la kijana Meshack Paka (20) kupoteza maisha na wengine wanne kujeruhiwa.

Aidha, raia wapatao 134 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, huku kukiwa na malalamiko ya kukosa huduma muhimu kama dhamana na matibabu.

CHADEMA imehimiza Jeshi la Polisi kujenga mahusiano mazuri na wananchi ili kuhakikisha usalama na kuzuia ghasia, ambapo Mnyawami ametoa wito kwa vyombo vya usalama kushughulikia kwa umakini matatizo yanayozua taharuki katika jamii, ili kudumisha amani na utulivu.

Pia, chama hicho kinaitaka serikali kuwaachilia huru raia waliokamatwa, na kuchunguza kwa kina chanzo cha matukio haya ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Katika tukio lingine, CHADEMA imeomba Jeshi la Polisi kuchunguza tukio la kijana Baraka Njile Makongolo ambaye alifariki dunia baada ya kudaiwa kushambuliwa akiwa mikononi mwa askari pia Chama hicho kimesisitiza umuhimu wa kuhakikisha haki inatendeka na kuwajibika kwa mujibu wa sheria.

CHADEMA pia imewapongeza wananchi wa Jimbo la Itilima kwa kujitolea kulinda usalama wao, na imetoa wito kwa wananchi wengine kuchukua tahadhari kwa ushirikiano na vyombo vya usalama.

CHADEMA Kanda ya Serengeti imetoa wito kwa pande zote zinazohusika kuhakikisha usalama na haki za wananchi zinaheshimiwa. Mnyawami amesema, “Tunasisitiza ushirikiano kati ya vyombo vya usalama na wananchi ili kudumisha amani na utulivu katika jamii zetu.”

Kanda ya Serengeti inajumuisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post