SIKU YA BAHARI AFRIKA; WANAWAKE SEKTA YA BAHARI WAASWA KULINDA MAZINGIRA

Na Grace Semfuko, Maelezo.

Wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya bahari nchini, wameungana na wanawake wenzao Duniani kuadhimisha siku ya bahari Afrika ambapo katika maadhimisho hayo wamesema ni muhimu kulinda mazingira ili kuwe na uchumi endelevu wa mazao katika sekta hiyo.

Wanawake hao leo Julai 27, 2024 wameadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi katika fukwe za Coco Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya bahari (WOMESA) Bi. Fortunata Kakwaya amesema wanaunga mkono juhudu za serikali za kulinda na kuendeleza gukwe za bahari ili kuweza kuwa na uchumi wa buluu imara na endelevu.

“Kama mjuavyo, kama bahari itachafuliwa hatutakuwa na mazingira safi ya bahari, kwa maana hiyo hatutakuwa na uchumi wa buluu endelevu, na ndio maana tumekuja kusafisha hii fukwe na kutoa elimu ili jamii ione umuhimu wa kulinda mazingira ya bahari, zoezi hili pia linalenga kuunga mkono juhudi za serikali za kuhifadhi mazingira” amesema Bi Kakwaya. 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Nelson Mlali amesema Tanzania kama taifa la lililozungukwa na neema ya maji linafanikisha kufanya biashara ya usafirishaji na nchi zingine, hivyo kuongeza pato la taifa. 

“Tunapoadhimisha tulio hili tunafanya kumbukumbu ya utajiri tuliopewa na Mwenyezi Mungu kama Bara la Afrika, kwa hapa Tanzania tumejaaliwa kuwa na maji na fukwe ndefu, yenye kilomita Zaidi ya 1,400, kupitia maji tunapata chakula na kufanikisha shughuli zetu za kiuchumi, sasa Tanzania kama taifa la maji tunafanikisha biashara sio tu ya nchi yetu lakini pia ya nchi zingine, katika Afrika nchi kama 32 zina ukanda wa pwani, zinapakana na bahari na theluthi ya nchi hizo hazihusiani na bahari, hasara wanazopata ni pamoja na kutumia mapato yao mengi ya nchi zaidi ya asilimia 40 kwa ajili ya kufanya biashara za kimataifa kupitia njia ya maji, kwa hiyo sisi kama nchi tumejaaliwa kuziepuka gharama hizo na badala yake pesa hiyo inatumika katika mambo mengine ya kijamii” amesema Bw. Mlali.

Nae Katibu Mkuu wa Chama cha Mabaharia Tanzania (TASU), Bw.Josiah Mwakibuja, amewataka mabaharia nchini kutoa taarifa pindi wanapokutana na viashiria vya uhalifu wawapo kwenye majukumu yao.

“Baharia ni mtu ambaye ana nidhamu na welezi, ni mtu ambaye amesoma, kuna baadhi ya masomo ambayo tunafundishwa mtu aweje katika meli au kwenye jamii, hao wanaoshiriki kufanya uhalifu ni wahalifu kama wahalifu wengine, na hao hawana weledi wa kibaharia, baharia ni mtu wa heshima, natoa wito tuwe na ushirikiano na vyombo vinavyohusika na usalama wa nchi , tuwe wepesi wa kutoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama pale tunapoona matukio ya uhalifu” amesema Bw. Mwakibuja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post